Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mataruma ya zege nchini, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya reli.

Serikali imewekeza Sh bilioni 379 katika kuboresha reli ya MGR kipande cha Kaliua–Mpanda chenye urefu wa kilomita 210, hatua inayolenga kuimarisha huduma za usafiri wa reli katika eneo hilo.

Profesa Mbarawa alitoa pongezi hizo jana alipokuwa akizungumzia uwekezaji huo katika eneo la Uyumbu, Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora. Alikuwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya miradi ya reli ya kisasa ya SGR katika vipande vya Makutopora–Tabora, Tabora–Isaka, Isaka–Mwanza na Tabora–Kigoma.

Alisema gharama ya kutengeneza taruma moja ya chuma ni takribani Sh 360,000, ikilinganishwa na Sh 130,000 kwa taruma moja ya zege inayozalishwa nchini, hali inayoonesha uwezekano wa kupunguza gharama kupitia matumizi ya teknolojia hiyo.

Aliongeza kuwa uzalishaji wa mataruma hayo nchini utajenga uwezo wa kitaalamu kwa Watanzania na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria. Aidha, hatua hiyo itafungua fursa kwa nchi jirani kunufaika na miundombinu ya reli ya Tanzania.

“Tunaamini kabisa huko tunakokwenda reli hii ya MGR nayo itakuwa ya kisasa na itafanya kazi kwa ufanisi na itasafirisha mzigo zaidi,” alisema Profesa Mbarawa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha mataruma yanayotosha kujenga kilomita 50 za reli kwa mwezi, sawa na kilomita 600 kwa mwaka.

Alisema matumizi ya mataruma ya zege ni sehemu ya mkakati wa kuboresha miundombinu ya reli na kuongeza uimara wa njia, hatua inayotarajiwa kuimarisha ufanisi wa usafirishaji.

“Tunaenda kuifanyia mapinduzi makubwa reli ya SGR kwa kubadilisha sasa kutoka kwenye mataruma ya chuma kuja kwenye haya ya zege,” alisema Mhandisi Shiwa.

Posted in

Leave a Reply