
Na Happy Milion
Watu wasiojulikana wanadaiwa kuiba transfoma katika Kijiji cha Mafinga, Kata ya Kipengere, Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe, tukio lililosababisha kukatika kwa huduma ya umeme katika Kitongoji cha Makela.
Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia Oktoba 24, 2026, majira ya saa tisa usiku, baada ya umeme kukatika ghafla na kuwafanya wananchi kudhani kuwa kulikuwa na hitilafu ya kawaida katika mfumo wa usambazaji wa umeme.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mafinga, Eses Chaula, alisema baada ya umeme kukatika, wananchi waliwasiliana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuomba msaada wa kurejesha huduma hiyo.
Alisema wataalamu wa TANESCO walipofika eneo la tukio na kufanya ukaguzi, walibaini kuwa transfoma ilikuwa imeshushwa kutoka kwenye nguzo na baadhi ya vifaa muhimu vilivyokuwa ndani yake kuondolewa.
“Umeme ulikatika ghafla, tukajua ni watu wa TANESCO, hivyo tukawapigia. Walipokuja kuangalia nguzo, wakabaini kuwa transfoma imeshushwa na vitu muhimu mle ndani vimeondolewa,” alisema Chaula.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Mohamoud Banga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, akisema Jeshi la Polisi limeanza msako wa kuwakamata watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na wizi huo.
Aidha, aliwataka wananchi kujiepusha na vitendo vya wizi na uharibifu wa miundombinu ya Serikali, ikiwemo ile ya TANESCO, akisisitiza kuwa vitendo hivyo huathiri utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
Leave a Reply