
Na George Gabriel
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma–Mangaka unaotekelezwa katika Kijiji cha Masuguru, Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, mkoani Mtwara.
Hafla ya uwekaji wa jiwe hilo la msingi imefanyika leo ikiwa sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo. Mradi huo umefikia asilimia 98 ya utekelezaji na unatarajiwa kunufaisha wananchi zaidi ya 81,000.
Mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 38.4 ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali katika sekta ya maji, unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, kupunguza changamoto ya uhaba wa maji na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.


Hadi sasa, huduma ya maji kupitia vioski na miunganisho ya majumbani imeanza kutolewa katika maeneo ya Masuguru, Nachura, Lidede, Mwambani, Sengenya, Mangaka, Kilimanihewa, Mkwajuni na Ngalinje.
Hatua hiyo inaonesha maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Maji kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma inayotolewa inakuwa endelevu.
Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kutunza na kulinda miundombinu ya maji pamoja na mazingira yanayozunguka vyanzo vya maji ili kuzuia uharibifu na kuhakikisha mradi huo unaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa muda mrefu.

Leave a Reply