Na Cosmas Msuha

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Msalato Satellite City unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo la Msalato jijini Dodoma.

Ziara hiyo ya ukaguzi ililenga kujionea maendeleo ya mradi huo wenye ukubwa wa takribani ekari 971, unaotarajiwa kutumika kwa shughuli mbalimbali za maendeleo na unatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na maeneo yanayozunguka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava, amepongeza juhudi zinazofanywa na wizara katika usimamizi wa sekta ya ardhi na kusisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendana na mipango ya serikali ya upimaji na upangaji bora wa ardhi.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo, aliishukuru kamati hiyo kwa kutembelea mradi na kupokea taarifa ya utekelezaji wake. Pia aliahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi, tija na kwa kuzingatia masilahi ya Taifa.

Aidha, Dkt. Akwilapo alisema mradi huo utasaidia kuongeza thamani ya ardhi, kuboresha mipango ya matumizi ya ardhi, kuvutia wawekezaji na kufungua fursa mpya za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka Uwanja wa Ndege wa Msalato.

Katika ziara hiyo, Waziri Akwilapo aliambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo Kaspar Mmuya, Katibu Mkuu Anthony Sanga pamoja na wajumbe wa menejimenti na wataalamu mbalimbali wa wizara hiyo.

Posted in

Leave a comment