Na Cartace Ngajiro, Tanga

Serikali ya Jamhuri ya Rwanda imesema itaendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Bandari ya Tanga pamoja na kuendelea kutumia bandari hiyo kupitishia mizigo yake.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba, alipofanya ziara katika Bandari ya Tanga kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa bandari hiyo na kutathmini fursa mbalimbali zinazopatikana.

Balozi Nyamvumba alisema Bandari ya Tanga ni kiunganishi muhimu katika usafirishaji wa mizigo ya kibiashara kwenda na kutoka Rwanda, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya pande hizo mbili.

Aidha, aliipongeza Bandari ya Tanga kwa huduma bora zinazotolewa katika kuhudumia mizigo ya Rwanda, jambo ambalo linaifanya nchi hiyo kuendelea kutumia bandari hiyo.

Awali, Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Peter Millanzi, alisema Rwanda ni miongoni mwa nchi zinazotumia Bandari ya Tanga kupitishia mizigo yake.

“Miongoni mwa bidhaa za Rwanda zinazopita katika Bandari ya Tanga ni pamoja na coil, magari, mitambo mbalimbali na mafuta,” alisema Millanzi.

Aliongeza kuwa Bandari ya Tanga imejipanga kuendelea kuboresha huduma kwa wateja wake ili kuvutia mataifa na wafanyabiashara wengi zaidi kutumia bandari hiyo.

Posted in

Leave a comment