Na Cosmas Msuha

Shughuli za uchimbaji madini katika Mgodi wa Namungo uliopo Wilaya ya Ruangwa zimeendelea kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hilo, huku wachimbaji waliokuwa wakihangaika kimaisha wakianza kunufaika na maendeleo kupitia sekta ya madini.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi wa Lindi, Dickson Joram alisema shughuli za uchimbaji katika mgodi huo zimechangia kuboresha huduma za maji, elimu, afya pamoja na miundombinu huku zikifungua fursa za ajira na kukuza biashara kwa wananchi wa maeneo yanayouzunguka mgodi huo.

Alieleza kuwa hali ya maisha ya wachimbaji na wananchi wa Namungo imebadilika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2019, ambapo wachimbaji wengi walikuwa wakitumia njia duni za uzalishaji na kushindwa kumudu mahitaji muhimu ya kila siku.

“Leo Namungo imebadilika kwa kiasi kikubwa, wananchi wanajitegemea na wanaendesha shughuli kubwa kupitia sekta ya madini,” alisema Mhandisi Joram.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa kampuni ya Elianje Limited, Joseph Shayo alisema kampuni hiyo ilianza shughuli za utafiti na uchimbaji mwaka 2020 na imekuwa ikihakikisha jamii inayozunguka mgodi inanufaika kupitia miradi mbalimbali ya kijamii.

Alisema kampuni hiyo imechimba visima na kusambaza maji katika Kijiji cha Tongwe pamoja na Kitongoji cha Namungo, huku ikiendelea kuboresha huduma ya maji safi na salama katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.

Katika sekta ya elimu, kampuni hiyo imejenga shule ya awali, kuboresha madarasa, kujenga vyoo vya kisasa na kushiriki katika ujenzi wa shule ya msingi katika Kitongoji cha Namungo ili kupunguza umbali wa wanafunzi kufuata elimu.

Aidha, mgodi huo umechangia uboreshaji wa barabara zinazounganisha vijiji na kata jirani pamoja na kusaidia shule mbalimbali kwa vifaa vya elimu ikiwemo kompyuta na mashine za uchapishaji.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Chingumbwa, Kata ya Mbekenyela Wilaya ya Ruangwa, Abdallah Manjakali alisema uwepo wa mgodi huo umefungua fursa nyingi za ajira, biashara na huduma za kijamii ambazo hapo awali zilikuwa changamoto kubwa kwa wananchi.

“Leo wananchi wanapata kipato na maisha yameimarika, pia kampuni imenunua gari la wagonjwa linalowahudumia wananchi bure wakati wa dharura bila kuchangishwa fedha yoyote,” alisema Manjakali.

Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya mgodi na jamii inayouzunguka unapaswa kuwa mfano kwa wawekezaji wengine wa sekta ya madini, huku akizitaka kampuni zenye leseni ambazo bado hazijaanza uzalishaji kuharakisha uwekezaji ili wananchi wanufaike zaidi na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.

Posted in

Leave a comment