
Na Cosmas Msuha
SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imeingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa maafa nchini kupitia matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Jim James Yonazi, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kujenga mifumo madhubuti ya kiutendaji inayoongozwa na maarifa, sayansi na teknolojia, ikiwemo matumizi ya Akili Unde (AI) katika kukabiliana na maafa.
Alisema makubaliano hayo yanatekeleza mapendekezo ya Mkutano wa Nane wa Umoja wa Mataifa wa Jukwaa la Dunia la Upunguzaji wa Vihatarishi vya Maafa uliofanyika Geneva, Uswisi, mwezi Juni 2025.
“Vyuo vikuu na taasisi za utafiti, ikiwemo Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, vina jukumu muhimu la kuzalisha maarifa na suluhisho za kisayansi zitakazosaidia kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa nchini,” alisema Dkt. Yonazi.
Alisema ili kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa makubaliano hayo, Serikali itaandaa mpango kazi wa utekelezaji pamoja na Ajenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Usimamizi wa Maafa, ambayo itabainisha maeneo ya kipaumbele yanayohitaji ufumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia.
Aidha, alisisitiza kuwa mafanikio ya makubaliano hayo yatapimwa kwa matokeo halisi yatakayochangia kuongeza usalama wa wananchi, kulinda rasilimali za taifa na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya maafa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Prof. Preksedis Marco Ndomba, alisema taasisi hiyo imeandika historia kwa kusaini makubaliano ya ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu, akibainisha kuwa mchakato wa kufanikisha ushirikiano huo ulianza muda mrefu na sasa umeanza kuzaa matunda.
“Tunaahidi kutekeleza na kufanikisha makubaliano haya kwa kuwa tuna uwezo na utaalamu wa kutosha. Tutaendelea kushirikiana katika masuala ya vihatarishi vya kitaifa ili kufanikisha adhima hii ya Serikali,” alisema Prof. Ndomba.

Ushirikiano huo unaelezwa kuendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inaweka msisitizo katika matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nguzo muhimu za maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii nchini.

Leave a comment