Na Cosmas Msuha

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekagua ujenzi wa Barabara ya Noranga (Doroto)–Itigi (Mlongojii) yenye urefu wa kilomita 25 inayojengwa katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida kwa gharama ya shilingi bilioni 29.6.

Dkt. Mwigulu amefanya ukaguzi huo leo wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Japherson Nnko.

Katika taarifa hiyo, Dkt. Mwigulu alielezwa kuwa hadi Mei 30, 2026, mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 83.25 ya utekelezaji ambapo kati ya kilomita 25 zinazojengwa, kilomita 20.2 zimekamilika kwa kiwango cha lami, huku kilomita 4.8 zilizobaki zikiwa zimefikia hatua ya tabaka la juu la msingi na zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026.

Mhandisi Nnko alisema kipande hicho ni sehemu ya Barabara ya Mbeya–Chunya–Makongolosi–Rungwa–Itigi–Mkiwa yenye urefu wa kilomita 524, inayounganisha mikoa ya Mbeya, Singida na Tabora na kwamba barabara hiyo inatarajiwa kuboresha usafirishaji wa watu, bidhaa na mazao katika ukanda huo hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi.

Aliongeza kuwa mradi huo unagharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania na unatekelezwa na Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) kwa gharama ya shilingi bilioni 29.6, bila kujumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kazi za ujenzi zilianza Septemba 16, 2022 na zinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2026 baada ya mkandarasi kuongezewa muda wa utekelezaji kwa mujibu wa masharti ya mkataba.

Hadi Mei 30, 2026, mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 12.9, huku akiidai Serikali shilingi bilioni 3.84. Aidha, Mhandisi Mshauri amelipwa shilingi bilioni 1.49 na anadai shilingi milioni 586.6.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa wananchi 578 walioathiriwa na utekelezaji wa mradi huo wamelipwa fidia ya jumla ya shilingi milioni 721.4 kwa mujibu wa sheria.

Katika utekelezaji wa mradi huo, jumla ya ajira 305 zimezalishwa, ambapo ajira 278 sawa na asilimia 91 zimetolewa kwa wazawa na ajira 27 sawa na asilimia 9 zimetolewa kwa wageni.

Posted in

Leave a comment