
Na Cosmas Msuha
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo amekutana na watanzania waishio Jamhuri ya Korea na kuwahimiza kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kuitangaza nchi na fursa mbalimbali katika sekta za uwekezaji, biashara na utalii.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika jana jijini Seoul, Balozi Dkt. Kombo alisema ni muhimu kwa watanzania kuifahamu vizuri nchi wanayoishi, ikiwemo tamaduni, lugha, sheria na mifumo ya kijamii ili waweze kujumuika na kujenga uhusiano chanya unaoweza kuleta manufaa kwa Taifa.
Balozi Dkt. Kombo aliwakumbusha kutumia majukwaa mbalimbali ya kitaaluma, kijamii na kibiashara kuitangaza Tanzania na fursa zinazopatikana katika nchi wanazoishi ili kuvutia wawekezaji, watalii na wadau wa maendeleo kushirikiana na Tanzania.
Aidha aliwaasa wanafunzi wa elimu ya juu nchini humo kujikita katika tafiti zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali nchini Tanzania hususan katika sekta za afya, maji, elimu na mazingira.
Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya watanzania nchini Korea, Eliusta Filikunjombe alieleza utayari wao wa kuendelea kushirikiana na serikali katika kutangaza fursa na kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea.

Balozi wa Tanzania nchini Korea, Mhe. Noel Kaganda alisema idadi ya watanzania nchini humo inafikia 300 ambayo inajumuisha wafanyakazi, wafanyabiashara na wanafunzi.
Balozi Dkt. Kombo yupo nchini Korea kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Korea na Afrika, unaolenga kuimarisha ushirikiano na mahusiano ya kidiplomasia, kiuchumi na maendeleo kati ya Korea na nchi za Afrika.
Leave a comment