
Na Jastini Bukebuke
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Louis Bura, amefunga rasmi mafunzo maalumu ya Ulinzi Shirikishi kwa washiriki 1,001 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Manispaa ya Geita, akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kuimarisha usalama na kulinda mali za umma na binafsi.
Hafla ya kufunga mafunzo hayo ilifanyika jana katika Viwanja vya GGM, Kata ya Kalangalala, mkoani Geita, ambapo Mhe. Bura alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa usalama.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Bura alisema mafunzo hayo yamewajengea washiriki uelewa na ujuzi wa kutekeleza dhana ya ulinzi shirikishi kwa ufanisi, ikiwemo mbinu za kukabiliana na vitendo vya uvamizi, wizi wa mawe ya madini na uhalifu mwingine unaolenga mali za GGML pamoja na maeneo mengine muhimu ya kiuchumi.
Alisema usalama wa jamii na uwekezaji ni msingi muhimu wa maendeleo, hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha amani na ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, alisema kuwa ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananchi na kwamba washiriki wa mafunzo hayo wamewezeshwa kushiriki kikamilifu katika kubaini, kuzuia na kupambana na vitendo vya uhalifu ndani ya maeneo yao.

Alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi endelevu za Jeshi la Polisi za kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola katika kudumisha amani, usalama na utulivu wa jamii.
Naye Mtendaji Mkuu wa GGML, Ashraf Suryaningrat, aliwapongeza wahitimu wote pamoja na Jeshi la Polisi kwa ushirikiano mkubwa uliofanikisha utekelezaji wa programu ya Ulinzi Shirikishi, akibainisha kuwa programu hiyo imeendelea kuleta matokeo chanya katika kuimarisha usalama wa mgodi na maeneo yanayouzunguka.

Suryaningrat alisema GGML itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na vyombo vya usalama katika kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kulinda rasilimali za taifa na kuchangia maendeleo ya jamii zinazozunguka mgodi.
Akihitimisha hafla hiyo, Mhe. Bura aliwataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuendelea kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao, kuongeza weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, kushiriki doria katika maeneo muhimu na kulinda miundombinu ya kimkakati.
Alisisitiza kuwa mazingira salama na yenye utulivu ni nguzo muhimu katika kuvutia uwekezaji, kukuza shughuli za kiuchumi na kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Geita na Taifa kwa ujumla.

Leave a comment