
Na Cartace Ngajiro, Tanga
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Mhe. Uzairu Athumani, ameipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Bandari ya Tanga, akisema umeongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia hadi meli 600 kwa mwaka na kufungua fursa nyingi za kiuchumi.
Mhe. Athumani alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya mafunzo katika Bandari ya Tanga, akiwa ameambatana na madiwani pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke. Ujumbe huo ulipokelewa na Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Athumani alisema wamevutiwa na historia, maendeleo na maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga, akieleza kuwa uwekezaji huo umeifanya bandari kuwa kitovu muhimu cha biashara na uchumi katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania.
“Kwa maelezo tuliyoyapata hapa, ni wazi kuwa Bandari ya Tanga ni mfano wa mafanikio ya uwekezaji wa kimkakati unaochochea ukuaji wa uchumi na kufungua fursa za biashara na uwekezaji,” alisema Mhe. Athumani.
Aliongeza kuwa lengo la ziara hiyo halikuwa kujifunza shughuli za bandari pekee, bali pia kutambua na kutathmini fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana ili kuona namna Halmashauri ya Temeke na wadau wake wanavyoweza kunufaika nazo.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega, alisema bandari hiyo imeendelea kupanua wigo wa huduma zake kwa kuhudumia masoko ya nchi jirani, ikiwemo Zimbabwe, huku matarajio yakiwa ni kuanza kuhudumia pia shehena za kutoka Sudan Kusini.
Alisema maboresho yaliyofanyika yameongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa bandari, ambapo kiwango cha shehena kinachohudumiwa kimeongezeka kutoka tani 700,000 hadi tani milioni mbili kwa mwaka huku kukiwa na ongezeko la meli zinazotia nanga kutokana na kuimarika kwa miundombinu na ufanisi wa huduma.
Bw. Mbega aliwahimiza madiwani na wadau wengine kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika miradi ya bandari kavu na shughuli nyingine zinazochochea ukuaji wa biashara na uchumi.


Leave a comment