Na Jastini Bukebuke

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, ameongoza maofisa na askari wa Jeshi la Polisi, wanachama wa Ulinzi Shirikishi pamoja na Geita Jogging Club kushiriki mazoezi maalumu yaliyoandaliwa na Idara ya Afya ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha maadhimisho ya Siku ya Sikoseli Duniani.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Glory Temba, alisema maadhimisho hayo yamelenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa sikoseli, athari zake, mbinu za kujikinga nao pamoja na kuhamasisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Dkt. Temba alisema kufanya mazoezi ya mwili kwa angalau dakika 30 kila siku ni muhimu katika kuboresha afya ya mwili na akili, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.

Aidha, aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuimarisha ustawi wa jamii na kuongeza tija katika shughuli za maendeleo.

Mazoezi hayo ya mchakamchaka yaliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya pamoja na wananchi, yakianzia Viwanja vya Kalangalala na kuhitimishwa katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Kalangalala.

Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa wito wa kuendeleza ushirikiano kati ya wadau mbalimbali katika kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa sikoseli, kuhamasisha uchunguzi wa afya na kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Posted in

Leave a comment