
Na Yusra Temba, Iringa
Msimu wa tano wa Great Ruaha Marathon umefanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha ukilenga kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kukuza utalii wa michezo.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Msajili wa Hazina na mlezi wa Great Ruaha Marathon, Nehemiah Mchechu, ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika hotuba yake, alisema uhifadhi wa mazingira una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
Alisema pia, Mto Ruaha Mkuu ni rasilimali muhimu inayochangia shughuli za kilimo, ufugaji na uzalishaji wa umeme, huku akiwahimiza watanzania kutembelea hifadhi za taifa na kushiriki katika juhudi za kuhifadhi maliasili.
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Gibril Mwishawa, alisema mbio hizo ni sehemu ya mkakati wa kuendeleza utalii wa michezo na kuitangaza Tanzania kupitia vivutio vyake vya kipekee vya utalii.
Kwa upande wake, Mratibu wa Great Ruaha Marathon, Hamim Kilahama, alisema marathon hiyo inalenga kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira na rasilimali za asili kupitia michezo

Msimu wa tano wa Great Ruaha Marathon umeandaliwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, wakiwemo Airtel Tanzania, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Maji ya Mkwawa, NMB Bank, Ununio Beach Park na Mkuu Creatives.

Leave a comment