Na Jastini Bukebuke

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Geita, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na watumishi kutoka idara mbalimbali za serikali, limeendesha msako maalum wa ukaguzi wa miundombinu ya umeme katika Mtaa wa Mwambageni, Kata ya Nyarugusu, Wilaya ya Geita.

Akizungumza wakati wa msako huo, Afisa Uendeshaji wa TANESCO Mkoa wa Geita, Elthemius Katemana, amewataka wakazi wa eneo hilo kuacha tabia ya kujiunganishia umeme kinyume cha sheria.

Alisema wananchi wanapaswa kufuata taratibu zilizowekwa na TANESCO ili kupata huduma ya umeme kwa njia halali, salama na endelevu.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, Abas Masune, akiwa ameambatana na wajumbe wa kata, alitembelea eneo hilo kujionea vitendo vya udanganyifu vilivyofanywa na baadhi ya wakazi kwa miundombinu ya umeme.

aliwawataka wananchi kuacha mara moja vitendo hivyo, akisisitiza kuwa vinahatarisha miundombinu ya umeme, usalama wa wananchi na vinaikosesha serikali mapato.

TANESCO imeeleza kuwa itaendelea kufanya operesheni kama hiyo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Geita na nchini kote kwa lengo la kudhibiti wizi wa umeme, kulinda miundombinu ya umeme na kuhakikisha matumizi ya nishati yanafuata sheria, taratibu na viwango vya usalama.

Posted in

Leave a comment