Na George Gabriel, Mtwara

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa Hospitali ya Mangaka iliyopo Wilaya ya Nanyumbu, mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wake kwa jamii na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Mashauli Elisante, alisema msaada huo unaonesha dhamira ya taasisi hiyo ya kushiriki katika maendeleo ya jamii sambamba na kutekeleza jukumu lake la kuzuia na kupambana na rushwa.

“Tunaamini afya bora ni msingi wa maendeleo ya jamii, na ni wajibu wa kila taasisi kushiriki pale inapowezekana katika kuboresha huduma zinazowagusa wananchi moja kwa moja,” alisema.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na magauni ya wajawazito na wazazi, viatu, vipima joto, sabuni pamoja na nepi za watoto (pampers), ambavyo vinatarajiwa kusaidia kuboresha huduma kwa akina mama, watoto na wagonjwa wengine wanaopatiwa huduma katika hospitali hiyo.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mangaka, Benedict Mbai, aliishukuru TAKUKURU kwa msaada huo, akisema vifaa hivyo vitasaidia kuboresha utoaji wa huduma na kupunguza changamoto zinazowakabili wahudumu wa afya, hususan katika wodi za akina mama na watoto.

Kwa upande wake, mmoja wa wazazi wanaopata huduma hospitalini hapo, Faudhia Geugeu, alitoa shukrani kwa TAKUKURU kwa msaada huo, akieleza kuwa umefika wakati muafaka na utanufaisha wananchi wengi wanaotegemea huduma za hospitali hiyo.

Msaada huo unaakisi umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta ya afya katika kuboresha ustawi wa wananchi na kuhakikisha huduma bora za afya zinaendelea kuwafikia Watanzania.

Posted in

Leave a comment