
Na Cosmas Msuha
Serikali imesema mageuzi yanayoendelea kutekelezwa katika sekta ya madini yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye mazingira bora ya uwekezaji barani Afrika, huku yakifungua fursa mbalimbali katika utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, uchakataji na uongezaji thamani wa madini.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, alitoa kauli hiyo jana alipofungua Kongamano la Madini lililofanyika katika Ukumbi wa Dome, ndani ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba.
Alisema maboresho ya sera, sheria na mifumo ya usimamizi wa sekta ya madini yameongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa sekta binafsi, hatua zilizochochea ongezeko la uwekezaji, ajira na mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Dkt. Kiruswa alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini, zikiwemo dhahabu, almasi, tanzanite, nikeli, makaa ya mawe, niobium, madini adimu pamoja na madini ya viwandani na ujenzi.
“Serikali haiwaaliki wawekezaji kuja kuchimba madini pekee, bali pia kuwekeza katika tafiti za kijiolojia, teknolojia za uchenjuaji, uchakataji, uongezaji thamani wa madini na viwanda vinavyotumia madini kama malighafi,” alisema Dkt. Kiruswa.
Akizungumzia kongamano hilo, alisema linatarajiwa kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji, huku akiwakaribisha wadau kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Madini utakaofanyika Novemba 19 hadi 21, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Alisema mkutano huo unalenga kuendelea kuitangaza Tanzania kama kitovu cha uwekezaji katika sekta ya madini barani Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini wa Tume ya Madini, CPA Venance Kasiki, alisema Tume inaendelea kusimamia utoaji wa leseni za utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na biashara ya madini kwa kuzingatia Sheria ya Madini ili kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha Watanzania na taifa kwa ujumla.
Alisema serikali pia inaendelea kuimarisha utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania, zinazolenga kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika usambazaji wa bidhaa na huduma ndani ya mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Aidha, aliwahimiza Watanzania kutumia fursa zilizopo kwa kuwekeza katika viwanda vinavyozalisha bidhaa na vifaa vinavyotumika migodini, pamoja na kutoa huduma mbalimbali zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji na uongezaji thamani wa madini.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Jumanne, alisema sekta ya madini imeendelea kutoa ajira kwa maelfu ya vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji.
Alisema serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama ili shughuli za uchimbaji zifanyike kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo, hatua itakayochochea maendeleo endelevu ya sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

Leave a comment