Na Cosmas Msuha

Wakazi wa Jiji la Dodoma wamesema ujenzi wa barabara za mzunguko umeleta manufaa makubwa kwao, ikiwemo kuongeza fursa za biashara, kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo yanayozunguka barabara hizo.

Mmoja wa wakazi wa eneo la Nala, Bi. Minnael Msanga, alisema uwepo wa barabara hiyo umeongeza idadi ya watu wanaopita katika eneo hilo na hivyo kuwapatia wakazi fursa zaidi za kufanya biashara.

Kwa upande wake, Mussa Rajab, mkazi wa Nala anayejishughulisha na kazi za ubebaji mizigo, alisema sehemu ya kisasa ya kuegesha magari iliyojengwa kandokando ya barabara imeongeza ajira na kipato kwao.

“Mwanzoni eneo hili halikuwepo, hivyo kusimama kwa magari hapa kulitegemea udharura wa dereva, nasi tulipata kazi kwa uchache sana. Lakini sasa magari yanasimama, mizigo inashushwa hapa na sisi tunapata ridhiki,” alisema Rajab.

Naye Simon Ndamanyilu, dereva wa lori la mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Rwanda, alisema barabara hiyo imewaondolea ulazima wa kupita katikati ya Jiji la Dodoma, jambo linalopunguza muda wa safari na matumizi ya mafuta.

“Imeturahisishia sana. Safari imekuwa fupi kwa sababu njia hii haina foleni hata kidogo,” alisema Ndamanyilu.

Akizungumzia mradi huo, Mhandisi Morice Mlay kutoka kampuni ya mzawa ya Inter-Consult Ltd, ambayo ni Mhandisi Mshauri wa mradi, alisema barabara za mzunguko zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dodoma, hasa malori yanayosafirisha mizigo kwenda nchi jirani.

Alisema sehemu ya kwanza ya mradi imefikia hatua za mwisho za utekelezaji na tayari imeanza kutumika, huku uzinduzi rasmi ukitarajiwa kufanyika Oktoba 2026 baada ya kukamilika kwa kazi zilizobaki.

“Ujenzi wa sehemu ya kwanza umefikia ukingoni. Kilichobaki ni baadhi ya kazi ndogo, ikiwemo ufungaji wa taa za barabarani na umaliziaji wa njia za watembea kwa miguu,” alisema Mhandisi Mlay.

Alifafanua kuwa mradi huo wa barabara ya njia nne kwa kiwango cha lami unaunganisha mikoa ya Morogoro, Arusha, Singida na Iringa. Barabara hiyo ina urefu wa kilometa 112.3, ambapo kipande cha kwanza chenye kilometa 52.3 kimekamilika kwa asilimia 93.3.

Mradi wa kipande cha kwanza unagharimu shilingi bilioni 100.84 na unatarajiwa kuendelea kuwa suluhisho la msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dodoma, huku ukichochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Dodoma, mikoa jirani na Taifa kwa ujumla.

Posted in

Leave a comment