
Na Cosmas Msuha
Serikali imewaagiza wazalishaji wote nchini kutumia alama ya ‘Made in Tanzania’ ili kuongeza utambulisho na imani kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, pamoja na kuimarisha ushindani wake katika masoko ya kimataifa.
Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Emmanuel Nchimbi, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Usiku wa Jubilei ya Dhahabu (Miaka 50) ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Makamu wa Rais alizitaka taasisi zinazosimamia viwango na huduma za kifedha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinakidhi viwango vinavyokubalika katika soko la kimataifa.
“Matumizi ya alama ya ‘Made in Tanzania’ yataongeza utambulisho wa bidhaa zenye ubora na kuimarisha heshima ya taifa katika biashara za kimataifa,” alisema Mhe. Balozi Nchimbi.
Aidha, aliwapongeza wadau wa sekta ya fedha kwa kuendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa viwanda vidogo na vya kati, akisema hatua hiyo imechangia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali na kuchochea ukuaji wa uzalishaji nchini.
Alisema Serikali itaendelea kuweka sera rafiki kwa uwekezaji, kuboresha miundombinu na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mbunge), alisema Tanzania itanufaika zaidi na rasilimali zake endapo itawekeza katika uchakataji na uzalishaji wa bidhaa za mwisho zenye thamani kubwa, badala ya kuendelea kuuza malighafi ghafi nje ya nchi.
Alibainisha kuwa hatua hiyo itafungua masoko mapya, kuongeza thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Mhe. Kapinga alisisitiza kuwa ili kujenga uchumi imara wa viwanda wenye ushindani, ni muhimu kubadili mtazamo wa uzalishaji kwa kuhakikisha mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini yanaongezewa thamani kwa kuchakatwa, kufungashwa vizuri na kuzalishwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Aidha, alisema uwekezaji katika teknolojia za kisasa una mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini, kupunguza gharama za uzalishaji na kuziwezesha bidhaa za Tanzania kushindana katika masoko ya kimataifa.
Hafla hiyo iliambatana na utoaji wa tuzo kwa washirika muhimu wa TANTRADE pamoja na taasisi zinazochangia maendeleo ya biashara, viwango na huduma za kifedha nchini.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Mhe. Balozi Nchimbi maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya TANTRADE ni fursa muhimu ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50, ikiwemo kuongezeka kwa viwanda, uzalishaji, ajira na upanuzi wa masoko ya bidhaa na huduma za Tanzania duniani.

Leave a comment