Na Mwandishi Wetu, DSM

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshauri kuwepo kwa mifumo bunifu ya kugeuza fursa za mazingira kuwa miradi inayotekelezeka, inayoweza kufadhiliwa na inayoweza kukua, ili kutengeneza fursa kwa kuunganisha wadau mbalimbali.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira wa Baraza hilo, Dkt. Careen Kahangwa, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Immaculate Sware Semesi, katika hafla ya kufunga Mkutano wa Tanzania Green Summit 2026 uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Alisema mfumo huo utasaidia kuwaunganisha wabunifu, wajasiriamali, jamii, wataalamu, teknolojia, masoko, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kufuatilia fursa zilizojadiliwa na kuendeleza ushirikiano ulioanzishwa, pamoja na kupima matokeo ya hatua zitakazochukuliwa baada ya kongamano hilo.

“Hatupaswi kuridhika kuona mawazo mazuri yakibaki kwenye mashindano, maonesho au miradi ya majaribio,” alisema Dkt. Kahangwa.

Alisema wakati umefika wa kuona mawazo hayo yakibadilika kuwa biashara endelevu, ajira, uwekezaji na suluhisho kwa changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, alisema ni muhimu kujenga ushirikiano wa kudumu utakaotafsiri maazimio ya kongamano hilo kuwa hatua na matokeo yanayopimika.

Alisisitiza kuwa Tanzania Green Summit isiwe tukio la siku mbili pekee, bali iwe sehemu ya mchakato endelevu wa kuunganisha sera, ubunifu, fedha, teknolojia na utekelezaji.

Tanzania Green Summit 2026 imefanyika kwa siku mbili, kuanzia Septemba 15 hadi 16, 2026, ikiwa na kaulimbiu “Turning Climate Action into Opportunity,” yenye maana ya “Kugeuza Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kuwa Fursa.”

Posted in

Leave a comment