Na Andrea Mlwafu

WAKALA wa Taifa wa Huduma za Ugani (NAESA) umewataka wakulima kutumia teknolojia za kisasa katika kuchakata mazao ili kupunguza upotevu, kuhifadhi virutubishi na kuongeza kipato kupitia bidhaa zenye thamani kubwa sokoni.

Wito huo ulitolewa wakati wa maonesho ya kitaifa ya kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika mkoani Tanga, ambapo NAESA ilionesha teknolojia mbalimbali za kilimo, ikiwemo uchakataji wa mpunga kwa kutumia mvuke.

Kaimu Meneja wa Sehemu ya Masoko na Uongezaji Thamani wa Mazao wa NAESA, Esther Mwaisango, alisema wakala huo unaratibu huduma za ugani na kuwawezesha maafisa ugani kupata maarifa na teknolojia zitakazowawezesha kuwafundisha wakulima mbinu bora za uzalishaji na uchakataji wa mazao.

Alisema katika maonesho hayo, wakufunzi kutoka vyuo vya mafunzo ya kilimo walionesha teknolojia zinazoweza kuwasaidia wakulima kuboresha ubora wa mazao yao na kukidhi mahitaji ya soko.

Alieleza kuwa kuwapatia maafisa ugani maarifa kuhusu teknolojia hizo kutasaidia wakulima kupata mafunzo ya vitendo kuhusu uchakataji, uhifadhi na uuzaji wa mazao kwa tija zaidi.

Mkufunzi kutoka Kituo cha Uhaulishaji Teknolojia za Kilimo cha MATI Ilonga, Morogoro, Hamis Abdalah Ramadhani, alisema teknolojia ya kuchakata mpunga kwa kutumia mvuke, inayojulikana kwa Kiingereza kama parboiling, husaidia kuhifadhi virutubishi na kupunguza kuvunjika kwa punje wakati wa kukoboa mchele.

Alisema teknolojia hiyo inahusisha maandalizi maalumu ya mpunga kabla ya kukobolewa, ikiwemo kutumia mvuke, ambao husaidia virutubishi kutoka katika tabaka la nje la punje kuelekea sehemu ya ndani.

Aliongeza kuwa teknolojia hiyo inaweza kuboresha ubora wa mchele na kumpa mkulima fursa ya kuuza bidhaa iliyoongezwa thamani badala ya kutegemea mauzo ya mpunga ghafi pekee.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, alizipongeza teknolojia zilizooneshwa, akisema matumizi ya teknolojia bora yana mchango mkubwa katika kuongeza tija ya kilimo na kuimarisha usalama wa chakula.

Burian aliwahimiza wakulima kutumia maonesho hayo kujifunza mbinu mpya na kupata taarifa zitakazowasaidia kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za kilimo.

Maonesho hayo yanalenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika mnyororo wa thamani wa mazao, kuanzia uzalishaji hadi uchakataji na uuzaji, ili kupunguza upotevu wa chakula na kuongeza kipato cha wakulima.

Posted in

Leave a Reply