
Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka Peter Kiariro, mkazi wa Maore, Wilaya ya Same, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Bernard Kiluwa (26), mkazi wa Kijiji cha Mheza, wilayani humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 12, 2026, katika Kitongoji cha Kalemane, Kijiji cha Mheza. Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa wivu wa kimapenzi.
Maigwa alisema kabla ya tukio hilo, marehemu alicheza muziki kwa muda mrefu na mke wa mtuhumiwa katika sherehe ya ubarikio iliyofanyika nyumbani kwa Shabani Rajab.
Alieleza kuwa baadaye, mtuhumiwa anadaiwa kumwomba marehemu waende pembeni kwa mazungumzo, lakini walipofika huko, alimshambulia kwa kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa kisu, na kumjeruhi tumboni na kifuani kabla ya kutoroka.
Marehemu alikimbizwa katika Kituo cha Afya Ndungu kwa ajili ya matibabu, lakini alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa huduma.
Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa huyo ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Aidha, Jeshi hilo limewaomba wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo kuzifikisha katika kituo cha polisi kilicho karibu.
Leave a Reply