
Na Happy Milion
Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, amemuondoa katika nafasi yake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Songwe, Mhandisi Fredrick Mande, na kumtaka kurejea makao makuu ya wakala huo jijini Dodoma.
Hatua hiyo ilichukuliwa usiku wa Oktoba 16, 2026, baada ya Waziri kutoridhishwa na usimamizi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Forodha–OSBP Tunduma, yenye urefu wa mita 1,675, mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Uamuzi huo umefuatia pia kutoridhishwa kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, na kasi ndogo ya ujenzi pamoja na kutotekelezwa kwa maagizo yake ya kufungua barabara zilizofungwa kutokana na mradi huo, hali inayowasababishia wananchi usumbufu wa usafiri.
Katika ziara ya kukagua mradi huo, Kadogosa alibaini changamoto za usimamizi na kumtaka mkandarasi kukamilisha kazi zilizobaki ndani ya majuma mawili.
Waziri huyo pia alisema atarejea eneo la mradi ndani ya siku saba kukagua utekelezaji wa maagizo yake na kuhakikisha kasi ya ujenzi inaongezeka.
Awali, Ndejembi alisisitiza kuwa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya miundombinu zinapaswa kuendana na maendeleo ya kazi. Alitaka TANROADS kuimarisha usimamizi na kuwachukulia hatua watendaji wanaoshindwa kutimiza wajibu wao au kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu utekelezaji wa miradi.
Baada ya ziara ya Songwe, msafara wa Makamu wa Rais ulielekea Mkoa wa Mbeya, ukitokea katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika Mkoa wa Rukwa.
Akiwa Mbeya, Ndejembi alieleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara ya Mbeya–Tunduma yenye njia nne, ambayo inatarajiwa kupunguza msongamano wa magari na changamoto za usafiri katika eneo hilo.
Pia, alieleza kutofurahishwa na usimamizi wa majukumu ya Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga. Hata hivyo, hatima ya nafasi yake bado inasubiri maamuzi, baada ya Makamu wa Rais kuelekeza hatua zichukuliwe dhidi ya watendaji wanaoshindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Kufuatia maelekezo hayo, Kadogosa amewaagiza mameneja wote wa TANROADS nchini kuhakikisha miradi ya barabara inasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji, huku kila upande ukitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mikataba.


Leave a Reply