
Na Andrea Mlwafu
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuweka mpango madhubuti wa usimamizi wa Dampo la Pugu Kinyamwezi ili kudhibiti athari za taka kwa afya za wananchi na mazingira.
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Pius Yanda, pamoja na wajumbe wengine wakati wa ziara ya kukagua hali ya mazingira katika dampo hilo iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Profesa Yanda amesema ni muhimu kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wananchi wanaoishi karibu na dampo hilo wanalindwa dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mrundikano wa taka, moshi na harufu. Ameipendekeza Halmashauri kuweka uzio kuzunguka eneo hilo kama sehemu ya kuboresha usalama na usimamizi wake.
Aidha, wajumbe wa kamati hiyo wamehimiza kufanyika kwa tathmini ya athari za kiafya zinazoweza kuwakabili wakazi wa maeneo jirani na dampo hilo, ili kubaini ukubwa wa changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana nazo.
Kamati pia imesisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa ujenzi wa madampo katika maeneo mengine kulingana na mahitaji, pamoja na kuhakikisha wazabuni wanaopewa jukumu la kukusanya taka wanakuwa na vifaa, rasilimali na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Ziara hiyo imelenga kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, Septemba 18, 2026, kuhusu kuboresha usimamizi wa taka katika Dampo la Pugu Kinyamwezi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha usimamizi wa taka na kuhakikisha zinageuzwa kuwa fursa za kiuchumi.
Kwagilwa amesisitiza umuhimu wa kumpata mwekezaji mwenye uwezo wa kusimamia shughuli za uchakataji wa taka katika dampo hilo, hatua inayotarajiwa kusaidia kupunguza athari za kiafya na kimazingira kwa jamii inayolizunguka.
Ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kushirikiana kwa karibu na taasisi zinazohusika na usimamizi wa mazingira, ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ili kuhakikisha dampo hilo linasimamiwa kwa kuzingatia misingi ya uendelevu na uhifadhi wa mazingira.
Katika ziara hiyo, kamati pia ilitembelea eneo la Mto Ng’ombe, wilayani Kinondoni, ambako ilipongeza juhudi za kuboresha mazingira ya mto huo, zikiwemo kazi za ujenzi wa kingo katika baadhi ya maeneo kwa lengo la kuimarisha uhifadhi wa mazingira.


Leave a Reply