Na Yusra Temba

UWANJA wa golf wenye mashimo 18, uliojengwa katika eneo la ekari 450 la Hifadhi ya Taifa Serengeti, umezinduliwa katika eneo la Fort Ikoma, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara, ukiwa na upekee wa kutokuwa na uzio ili kuruhusu wanyamapori kuendelea kutumia eneo hilo kwa uhuru.

Uwanja huo wenye jumla ya Par 72 unatarajiwa kupanua wigo wa utalii wa michezo nchini na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa, kwa kuunganisha mchezo wa golf na uzoefu wa kutazama wanyamapori katika mazingira yao ya asili.

Akizindua uwanja huo jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alisema Serikali inaendelea kubuni bidhaa mpya za utalii ili kuongeza mvuto wa nchi kwa wageni wa ndani na nje.

“Serikali imeendelea kuweka mkazo katika ubunifu wa mazao mapya ya utalii yatakayoongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa,” alisema.

Aliongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa wanyamapori na michezo barani Afrika.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa, alisema uwanja huo unalenga kuongeza thamani ya vivutio vya nchi na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi, zikiwemo ajira, biashara na utoaji wa huduma katika maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo.

Uwanja huo pia umewekewa mfumo wa umwagiliaji wa maji ardhini unaolenga kusaidia utunzaji wa eneo la mchezo na kupunguza athari kwa mazingira, huku shughuli zake zikizingatia taratibu za uhifadhi.

Naye Robinson Owiti, mchezaji wa kulipwa wa golf kutoka Kenya, alisema amefurahishwa na fursa ya kucheza katika uwanja huo, akieleza kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kutembelea Serengeti na kushuhudia wanyamapori katika makazi yao ya asili.

Uzinduzi huo ulipambwa na burudani mbalimbali, zikiwemo ngoma za asili na muziki.

Uwanja huo unaongeza aina ya shughuli zinazoweza kuvutia watalii Serengeti, huku ukitoa fursa ya kukuza utalii wa michezo sambamba na kuendeleza uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

Posted in

Leave a Reply