
Na Mwandishi Wetu, Nachingwea – Lindi
MNADA wa kwanza wa korosho wa msimu huu uliofanywa na Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI umezalisha mauzo ya kilo 10,830,000 za korosho zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 36, huku bei ya juu ikifikia Shilingi 3,410 kwa kilo na bei ya chini ikiwa Shilingi 3,270.
Matokeo hayo yaliyopatikana jana katika makao makuu ya RUNALI wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi, yameweka mwanzo wenye matumaini kwa msimu huu wa korosho, huku wakulima wakieleza kuridhishwa na bei zilizopatikana, wakizitaja kuwa nzuri ikilinganishwa na msimu uliopita.
Akizungumza katika mnada huo akiwa mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, aliipongeza Serikali kwa juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo, huku akiwataka wakulima na wadau wa korosho kuongeza uzalishaji ili kufikia lengo la tani 300,000.
Malima alisema mapato yanayotokana na zao hilo yana mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya wananchi na kukuza uchumi kupitia shughuli za kilimo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, alisema wilaya hiyo inalenga kuzalisha korosho zenye ubora wa daraja la kwanza (Grade A), akisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora katika hatua zote za uzalishaji na utunzaji wa zao hilo.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha sifa ya korosho za Nachingwea na kuongeza ushindani wake katika soko.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred, aliwahimiza wakulima kudumisha ubora wa korosho, kuzipeleka sokoni kwa wakati na kuzihifadhi katika mazingira yanayokidhi viwango vinavyotakiwa ili kupata bei nzuri.
Pia alisisitiza umuhimu wa kukagua korosho zilizohifadhiwa maghalani na kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mwenyekiti wa RUNALI, Odas Mpunga, aliwataka wakulima kupeleka korosho zao sokoni kwa wakati na kuzingatia taratibu za uuzaji ili kuhakikisha wananufaika ipasavyo na zao hilo.
Mauzo hayo ya mnada wa kwanza yanaweka matarajio mapya kwa wakulima wa korosho mkoani Lindi, huku juhudi za kuongeza uzalishaji, kudumisha ubora na kuimarisha masoko zikitarajiwa kuwa muhimu katika kuongeza kipato cha wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.


Leave a Reply