Na Andrea Mlwafu

Serikali imeimarisha mkakati wa kuwashirikisha wasanii, waigizaji, wanamichezo na watengeneza maudhui katika kutoa elimu kwa umma kuhusu historia, chimbuko na misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hususan kwa vijana.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema hayo leo, jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya ofisi hiyo na wadau hao kilicholenga kujadili mpango wa kutoa elimu ya Muungano kwa umma.

Amesema wasanii na watengenezaji wa maudhui wana uwezo mkubwa wa kuhamasisha jamii kupitia majukwaa yao, ikiwemo mitandao ya kijamii na kwamba ushiriki wao utasaidia kuifikisha elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

Alisema elimu ya Muungano ni ajenda ya kudumu inayolenga kukuza uelewa wa Watanzania kuhusu historia yao, walikotoka, walipo na wanakoelekea kama taifa na kusisitiza umuhimu wa kutumia vipaji vya wasanii katika kuimarisha na kuenzi misingi ya Muungano.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Muungano katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Latifa Mohammed Khamis, alisema kuwashirikisha wasanii na watengenezaji wa maudhui kutoka pande zote mbili za Muungano ni miongoni mwa mikakati ya kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.

Katika kikao hicho, mwimbaji wa taarab Hadija Omary Kopa na wadau wengine wamepongeza mpango huo na kueleza utayari wao wa kutumia akaunti zao za mitandao ya kijamii kutoa elimu kuhusu Muungano, hususan kwa vijana wanaowafuatilia.

Wadau hao pia wamependekeza wanamuziki kuandaa nyimbo maalumu za kuhamasisha uzalendo na kuenzi Muungano, sambamba na kuimarisha utoaji wa elimu hiyo katika taasisi za elimu, kuanzia shule za msingi hadi vyuo.

Wakirejelea takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, wadau hao wamesema kuwa asilimia 77.3 ya Watanzania walizaliwa baada ya kuasisiwa kwa Muungano, hivyo kufanya elimu kuhusu historia na misingi yake kuwa muhimu kwa vizazi hivyo.

Kikao hicho cha siku moja kimewashirikisha wasanii, waigizaji na watengeneza maudhui, wakiwemo Victor Victor, maarufu Nanga; Mohamed Mwinchande, maarufu Matofali; Ester Luckson, maarufu Mama Chanja; Amani Nzala Nzala; Vicent Njau, maarufu Kiredio; Fredrick Bundala, maarufu Sky Walker; na John Rojas, maarufu Simple the Boy.

Posted in

Leave a Reply