Na Mwandishi Wetu

Serikali imezitaka halmashauri nchini kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuweka na kuuza vitabu vinavyoenzi utamaduni wa Kitanzania, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa vitabu, kukuza utamaduni wa kusoma na kuongeza soko la machapisho ya ndani.

Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Nne la Kitaifa la Huduma za Maktaba, Tamasha la Vitabu na Usomaji, pamoja na Mfumo Jumuishi wa Maktaba Mtandao wa Taifa (INDLS), uliofanyika katika viwanja vya Maktaba Kuu jijini Dar es Salaam.

Profesa Mkenda amesema usomaji wa vitabu ni nyenzo muhimu katika kukuza maarifa, kujenga maadili na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu masuala mbalimbali yanayochangia maendeleo ya taifa.

Amesema kutengwa kwa maeneo maalumu ya vitabu katika halmashauri na nyumba za ibada kutarahisisha upatikanaji wa machapisho kwa wananchi, huku kukiwapa waandishi na wachapishaji fursa zaidi za kusambaza na kuuza kazi zao.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono waandishi wa vitabu nchini kwa kuweka mazingira yatakayochochea ukuaji wa soko la vitabu, ikiwemo kuongeza fursa za usambazaji na ununuzi wa machapisho yao.

Aidha, amesema ushiriki wa taasisi mbalimbali ni muhimu katika kujenga jamii inayothamini usomaji na kutumia maarifa yanayopatikana kupitia vitabu katika maisha ya kila siku.

“Ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za kidini na wadau wa sekta ya vitabu unaweza kusaidia kueneza machapisho yanayohusu historia, lugha, mila na desturi za Kitanzania, pamoja na maarifa yanayochochea maendeleo ya jamii,” amesema Profesa Mkenda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dk. Mboni Ruzegea, amesema kongamano hilo linajadili masuala mbalimbali yanayohusu uboreshaji wa huduma za maktaba, yakiwemo Mfumo Jumuishi wa Maktaba Mtandao wa Taifa (INDLS), sheria na sera, taaluma ya maktaba pamoja na ushirikiano na taasisi za Serikali.

Amesema majadiliano hayo yanalenga kuimarisha utoaji wa huduma za maktaba na kupanua fursa za wananchi kupata taarifa na maarifa kupitia mifumo ya kisasa.

Ameongeza kuwa kongamano hilo limewakutanisha wadau wa huduma za maktaba, waandishi, wasomaji na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kujadili namna teknolojia za kidijitali zinavyoweza kupanua upatikanaji wa taarifa, kukuza ujuzi na kuchangia maendeleo endelevu.

Posted in

Leave a Reply