Sehemu ya washarika wakiisikiliza Kwaya ya Uinjilisti KKKT Mtaa wa Kwembe wakati wa ibada leo, (Picha na Vincent Mpepo)

Na Vincent Mpepo

Wakristo wametakiwa kuwa wavumilivu wanapokutana na changamoto mbalimbali za maisha huku wakiendelea kumtegemea Mungu kwa kuwa matatizo wanayopitia hayapaswi kuwakatisha tamaa wala kuwafanya waache kumtanguliza Mungu katika maisha yao.

Wito huo umetolewa leo na Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa wa Kwembe, Emeline Mnzava, wakati akihubiri katika kanisa hilo, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuvumilia katika nyakati ngumu na kubaki katika kusudi la Mungu.

Alisema kuwa katika maisha ya kila siku mwanadamu hukutana na changamoto mbalimbali zinazohitaji uvumilivu, imani na kumtegemea Mungu, ambaye ndiye kimbilio la kweli katika nyakati zote.

Aidha, aliwataka waumini kutenda mema na kumtanguliza Mungu katika kila jambo wanalolifanya ili waendelee kuishi katika ulinzi wake, akisisitiza kuwa hawapaswi kukata tamaa kwa sababu Mungu hajawahi kumwacha anayemtegemea.

Akifafanua zaidi, alitoa mfano wa Yusufu wa kwenye Biblia ambaye alipitia changamoto nyingi, ikiwemo chuki na vitendo vya ndugu zake, lakini aliweza kushinda kutokana na kudumu katika imani na kumtegemea Mungu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa kanisa hilo, Exaud Mchome, alitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi na kuwashukuru waumini pamoja na jumuiya mbalimbali kwa kuendelea kutoa sadaka za ujenzi, akisema kuwa shughuli za ujenzi zinaendelea vizuri.

“Tunamshukuru Mungu mpaka sasa uwekaji wa sakafu (tiles) ndani umekamilika na tunaendelea kuwakumbusha ambao bado hawajatoa michango wafanye hivyo ili tukamilishe na sehemu ya nje,” alisema Mchome.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Yerusalemu, Michael Mwambage, alisema katika zoezi la utoaji wa sadaka ya mavuno, jumuiya hiyo imewashirikisha hadi watoto, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuwajengea utamaduni wa kutoa tangu wakiwa wadogo.

Sehemu ya Wanakwaya ya Uinjilisti ya KKKT Kwembe ikihudumu leo katika ibada

Aidha, aliwashukuru viongozi wenzake, walezi wa jumuiya hiyo na wanajumuiya wote kwa ushirikiano wao uliofanikisha malengo ya utoaji wa sadaka katika jumuiya yao.

Posted in

Leave a Reply