Screenshot

Na Juma John Elisha

Mahakama Kuu ya Tanzania imemhukumu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kifungo cha miaka minne jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Novemba 6, 2026, na jopo la majaji watatu lililoongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

Aidha, Mahakama imemweleza Lissu kuwa ana haki ya kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Lissu alisisitiza kuwa hakuwa tayari kuomba msamaha kwa sababu anaamini hana hatia.

Lissu alipinga kutiwa hatiani kwa kosa la uchochezi, akieleza kuwa shtaka alilokuwa akikabiliwa nalo katika kesi hiyo lilikuwa la uhaini.

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, kufuatia hotuba aliyoitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma na baadaye alisafirishwa kwenda Dar es Salaam na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 10, 2025, ambako alisomewa shtaka la uhaini.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa mahakamani, Lissu alikuwa amekaa mahabusu kwa takribani mwaka mmoja na miezi saba akisubiri kukamilika kwa mwenendo wa kesi hiyo.

Akizungumza kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Lissu alisema kuwa siku hiyo ilikuwa ni siku yake ya 577 akiwa mahabusu.

Hukumu hiyo inaashiria hatua nyingine muhimu katika kesi iliyokuwa ikifuatiliwa kwa karibu na wadau mbalimbali wa masuala ya siasa, demokrasia na haki nchini Tanzania.

Posted in

Leave a Reply