
Na Mwandishi Wetu, Songea
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Juhudi iliyopo Kata ya Ruvuma, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia nidhamu na kujituma katika masomo ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu na kuwa raia bora wa baadaye.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Songea, Mkaguzi wa Polisi Koladina Mahundi, Aprili 15, 2026, alipofanya ziara shuleni hapo kwa lengo la kutoa elimu ya ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya usalama.
Mahundi, ambaye aliambatana na Polisi Kata ya Ruvuma, Mkaguzi wa Polisi Frank Makuwa, alisema nidhamu ni msingi muhimu katika kufanikisha malengo ya wanafunzi, huku akiwahimiza kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu mustakabali wao.
Aliongeza kuwa wanafunzi ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili, hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuripoti viashiria vya matukio hayo kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Kwa upande wake, Mkaguzi Makuwa aliwataka wanafunzi kuepuka utoro na mahusiano ya kimapenzi wakiwa shuleni, akisisitiza kuwa tabia hizo ni kinyume na maadili na zinaweza kuathiri masomo yao na ndoto zao za baadaye.

Leave a comment