
Na Cosmas Msuha
Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano wa kibunge kimataifa kupitia ushiriki wake katika Mkutano wa 5 wa Mabunge ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM-PN).
Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo (MB), akimwakilisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, alitoa msimamo huo wakati wa mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Hilton Istanbul, nchini Uturuki, Aprili 15, 2026.

Katika mkutano huo, Mhe. Sillo alieleza kuwa Bunge la Tanzania linaunga mkono azimio la kulipa hadhi Bunge la Kiarabu kuwa mwangalizi katika Umoja wa Mabunge ya nchi hizo, hatua inayolenga kupanua wigo wa ushirikiano wa kibunge kimataifa.
Alibainisha kuwa Tanzania inatambua umuhimu wa kuendeleza uhusiano na taasisi za kimataifa kama sehemu ya kuimarisha taasisi za kibunge na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya NAM-PN.
Katika ziara hiyo, Mhe. Sillo aliambatana na Mbunge wa Singida Mashariki, Mhe. Elibariki Kingu, ambapo walishiriki kikamilifu katika majadiliano ya mkutano huo.
Kwa mujibu wa azimio hilo, Bunge la Kiarabu sasa litashiriki vikao na shughuli za NAM-PN kama mwangalizi, baada ya ombi lake rasmi kukubaliwa na nchi wanachama. Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kibunge na kukuza malengo ya pamoja ya nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote.
Uamuzi huo unaonesha dhamira ya Tanzania katika kujenga na kuendeleza ushirikiano na nchi za Kiarabu pamoja na jumuiya nyingine za kimataifa kwa maslahi ya maendeleo ya pamoja.

Leave a comment