Na Cosmas Msuha

Katika juhudi za kudumisha amani, mshikamano na maendeleo ya taifa, vijana wametakiwa kuwa wakakamavu, wazalendo na kuichukia rushwa inavyochangia mmomonyoko wa maadili nchini.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, wakati akizindua programu ya “Vijana Plattform” iliyoambatana na semina ya makundi mbalimbali ya vijana katika Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam kuanzia Aprili 13 hadi 14, 2026.

Akizungumza katika hafla hiyo, Msando alisema serikali kupitia programu ya “Vijana Tuijenge Tanzania Yetu” inalenga kuwaandaa vijana kwa ajira endelevu, pamoja na kuboresha huduma za afya hasa kwa mama na mtoto kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

“Hakikisha unalinda usalama wa nchi yako. Uzalendo wa kweli ni kuipenda nchi, kutoa taarifa sahihi na kuwa raia mwema,” alisema Msando.

Alisema kupitia sera ya ajira, serikali imepanua wigo wa upatikanaji wa elimu kwa kujenga shule katika kila kata, pamoja na kutoa ajira na mikopo yenye riba nafuu kwa zaidi ya vijana laki tisa.

Kwa upande wake, Afisa Vijana wa Manispaa ya Ubungo, Allen Mjindo, aliipongeza serikali kwa kuandaa kongamano hilo, akisema litawawezesha vijana kutambua na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao.

“Kongamano hili linawaleta pamoja vijana wa kada mbalimbali kama wanafunzi, bodaboda, wanasiasa na wafanyabiashara ili kushirikiana katika kujenga taifa,” alisema Mjindo.

Diwani wa Kata ya Mbezi, Pius Nyatori, alisema mafunzo hayo yatawasaidia vijana kuelewa vizuri namna ya kunufaika na mikopo ya halmashauri yenye riba nafuu, ambayo ni chachu muhimu ya maendeleo yao kiuchumi.

“Kijana unatakiwa kujifunza kutengeneza vitega uchumi na kutumia fursa ipasavyo; ukifanya hivyo, fedha itakufuata,” alisisitiza Nyatori.

Kwa upande wake, mama mjasiriamali kutoka Kata ya Mbezi, Elizabeth Ngonera, alisema vijana wakijitambua na kutumia vizuri fursa zilizopo, wanaweza kubadilisha maisha yao na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa.

Ngonera alishauri kuwepo kwa ushirikiano kati ya serikali, wazazi na jamii ili kufanikisha  jukumu la kuwawezesha vijana kwa kuwapatia elimu, mafunzo na mazingira rafiki yatakayowawezesha kukuza uchumi wao binafsi, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla.

Posted in

Leave a comment