
Na Cosmas Msuha
Ofisi ya Waziri Mkuu imewawezesha watu wenye ulemavu kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kupitia Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA).
Ushiriki huo umewawezesha kuonesha bidhaa na huduma mbalimbali wanazozalisha na kuzitoa, pamoja na kufanya biashara katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Akitembelea mabanda ya washiriki hao, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, alieleza kuridhishwa na kiwango cha ushiriki wa watu wenye ulemavu, akibainisha kuwa ushiriki wao umeongeza fursa za kiuchumi na kuonesha uwezo wao katika uzalishaji na biashara.
Aidha, Nderiananga aliipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na taasisi nyingine zilizowezesha ushiriki huo na kuzitaka mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kutenga na kutoa mikopo ya asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi.
“Ni wakati sasa kwa watu wenye ulemavu kuendelea kuonesha uwezo wao katika uzalishaji na biashara. Kupitia maonesho haya tumejionea matokeo chanya ya uwezeshaji wa kiuchumi unaotokana na mikopo na fursa zinazotolewa na Serikali,” alisema Nderiananga.
Kwa upande wake, mwakilishi wa washiriki hao, Bi. Pili Bilahi, aliishukuru Serikali kwa kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo bila kulipia gharama yoyote.
Vilevile, Bi. Bilahi aliishukuru serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yanayowapa watu wenye ulemavu fursa za kiuchumi, ikiwemo kupitia mikopo ya asilimia mbili ya mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri.
Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanaendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere chini ya kaulimbiu isemayo, “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ni Fahari ya Tanzania,” yakilenga kukuza biashara, uwekezaji na ubunifu nchini. Maonesho hayo yalianza Juni 28 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026.


Leave a comment