
Na Cosmas Msuha
Mjiolojia kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Abbas Mruma, amesema Tanzania inaendelea kujijengea nafasi muhimu duniani kutokana na kuwa na hifadhi kubwa ya madini ya kimkakati, yakiwemo graphite, lithium na rare earth elements, ambayo ni nguzo muhimu katika maendeleo ya teknolojia za kisasa na nishati safi.
Mruma alitoa kauli hiyo wakati akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Stanslaus Muyungi, alipotembelea banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Alisema mahitaji ya madini ya lithium yanaongezeka kwa kasi duniani kutokana na matumizi yake katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, simu za mkononi, kompyuta mpakato na vifaa vingine vya kisasa vya kielektroniki.
Kwa mujibu wa Mruma, nchini Tanzania madini ya lithium yanapatikana zaidi katika maeneo ya Dodoma na Ikungi, mkoani Singida, hali inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya kunufaika na ongezeko la mahitaji ya madini hayo katika soko la kimataifa.
Akizungumzia madini ya graphite, alisema Tanzania ndiyo nchi inayoongoza barani Afrika kwa kuwa na hifadhi kubwa ya madini hayo, ambayo ni malighafi muhimu katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme pamoja na matumizi mbalimbali ya viwandani.
Aidha, alisema Tanzania pia ina hifadhi kubwa ya madini ya rare earth elements katika Ukanda wa Afrika Mashariki, yanayopatikana katika eneo la Ngualla mkoani Songwe na Wigu mkoani Morogoro. Madini hayo yanatumika katika utengenezaji wa vifaa vya teknolojia ya juu, ikiwemo vifaa vya mawasiliano, nishati jadidifu na vifaa vya ulinzi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Stanslaus Muyungi, aliipongeza Tume ya Madini kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu rasilimali za madini na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.
Alisema elimu hiyo ina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa rasilimali za madini, kuvutia uwekezaji na kuonesha nafasi ya sekta ya madini katika kukuza uchumi na kufanikisha maendeleo endelevu ya Taifa.


Leave a comment