Na Jastini Bukebuke

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Chato, Lufuta Magoma (40), mganga wa kienyeji na mkazi wa Kijiji cha Rutunguru, akikabiliwa na shtaka la kumuua mama yake mzazi, Dotto Magoma Nyara (70).

Mshtakiwa alipandishwa kizimbani jana, Julai 10, 2026, ambapo alisomewa shtaka la mauaji mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Erick Kagimbo.

Akisoma shauri la jinai namba 15471/2026, Wakili wa Serikali, Mashaka Said, alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 4, 2026, katika Kijiji cha Rutunguru, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa Lufuta Magoma alimuua mama yake mzazi, Dotto Magoma Nyara, kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Hata hivyo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu shtaka hilo kwa kuwa Mahakama ya Wilaya haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Hakimu Kagimbo alisema kuwa kutokana na aina ya shtaka linalomkabili mshtakiwa, kesi hiyo haina dhamana, hivyo ataendelea kuwa mahabusu hadi upelelezi utakapokamilika na hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa.

Kesi hiyo imeahirishwa mpaka Julai 23, 2026, kwa ajili ya kutajwa, huku mshtakiwa akirejeshwa rumande akisubiri maendeleo ya upelelezi.

Posted in

Leave a comment