Na Cosmas Msuha

KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Dkt. Sophia Nchimbi, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, amezindua mradi wa Mama Tembe unaolenga kuhifadhi urithi wa kiutamaduni wa Wagogo, kuwawezesha wanawake na wasichana, pamoja na kukuza uchumi kupitia ubunifu wa asili.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika hivi karibuni wilayani Chamwino, mkoani Dodoma. Mradi unasimamiwa na Shirika la Innovation Development for Future Generation (IDFG) kwa ufadhili wa Serikali za Uswisi na Norway kupitia programu ya Articipate.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Nchimbi alisema mradi unawahusisha wanawake wazee 15 wa kabila la Kigogo, mabinti 20 na wanafunzi kutoka shule tatu ambao watarithi mbinu za uchoraji wa jadi kwa kutumia zana na malighafi za asili zilizokuwa zikitumika kupamba nyumba za tembe.

Alisema uchoraji wa nyumba za tembe si mapambo ya kawaida bali ni sehemu muhimu ya historia na utambulisho wa Wagogo, hivyo kurejeshwa kwake kutasaidia kuitangaza Chamwino kama kitovu cha utalii wa utamaduni kupitia kazi za ubunifu zinazofanywa na wananchi.

“Tunafungua ukurasa mpya wa kuhifadhi utamaduni wetu. Kupitia mradi huu, Chamwino itanufaika kwa kuitangaza historia na utamaduni wake,” alisema Dkt. Nchimbi.

Aliongeza kuwa mradi huo pia utawawezesha wananchi kujiongezea kipato kupitia shughuli za sanaa, huku Halmashauri ikiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha unafanikiwa.

Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Chamwino, Jackson Kitija, alisema mradi umefika kwa wakati muafaka kwani baadhi ya maarifa ya jadi yalikuwa yameanza kupotea kutokana na wazee waliokuwa nayo kuzeeka huku vijana wengi wakikosa fursa ya kuyajifunza.

Kitija alisema hatua inayofuata ni kuhakikisha ubunifu wa wanawake hao unalindwa kwa kupata hati miliki, huku michoro hiyo ikitumika kutengeneza bidhaa mbalimbali zenye thamani ya kiuchumi, ikiwemo mavazi yatakayobeba utambulisho wa sanaa ya Wagogo.

Mkurugenzi wa Shirika la Innovation Development for Future Generation (IDFG), Bi. Victoria Mponda, alisema mradi wa Mama Tembe umebuniwa baada ya utafiti kubaini kuwa wanawake wa Kigogo walikuwa na mchango mkubwa katika kuhifadhi utamaduni kupitia michoro ya nyumba za tembe.

Alisema mradi hautaishia kutoa mafunzo pekee, bali utakusanya historia ya michoro hiyo, kueleza maana ya kila mchoro na kuhifadhi taarifa zote kidijitali ili ziwe rejea kwa vizazi vijavyo.

“Tunataka wanawake hawa watambulike kama wabunifu wa sanaa hii. Tutahifadhi kazi zao kidijitali, tutazisajili kwa hati miliki na baadaye kuzigeuza kuwa bidhaa zitakazoweza kuuzwa,” alisema Mponda.

Alieleza kuwa changamoto kubwa mwanzoni mwa utekelezaji wa mradi ilikuwa kuwashawishi wanawake wazee kushiriki, kwa kuwa wengi hawakuamini kuwa uchoraji walioutumia kwa miaka mingi kupamba nyumba ungeweza kuwa chanzo cha kipato.

“Kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na wa kimila tuliwafikia na kuwajengea uelewa kuwa sanaa nayo ni uchumi. Leo wamekubali kurithisha maarifa yao kwa mabinti, jambo ambalo tunaamini litakuwa mwanzo wa kufufua sanaa iliyokuwa ikielekea kutoweka,” alisema Mponda.

Miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ni Bi. Esteli Chibaya (84), mkazi wa Chamwino, ambaye alisema amefurahishwa na hatua ya kupewa nafasi ya kurithisha ujuzi alioupata tangu akiwa msichana, akiamini kuwa vijana wataendelea kuuenzi utamaduni wa Wagogo badala ya kuuacha upotee.

“Tulikuwa tunachora nyumba kwa ajili ya kuzipamba bila kujua kuwa siku moja ujuzi huu ungekuwa sehemu ya maendeleo yetu. Leo nina furaha kuona watoto na wajukuu wetu wataurithi na kuutumia kujenga maisha yao,” alisema Bi. Chibaya.

Mradi wa Mama Tembe unatarajiwa kukamilika Oktoba 2026. Wadau wanaamini kuwa, mbali na kufufua sanaa ya uchoraji wa nyumba za tembe, utasaidia kuhifadhi urithi wa kabila la Wagogo, kuimarisha utalii wa utamaduni na kuwawezesha wanawake kutumia maarifa ya jadi kama nyenzo ya kujiletea maendeleo.

Posted in

Leave a comment