
Na Jastini Bukebuke, Geita
Afisa Tawala wa Wilaya ya Geita, Lucy Beda, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashimu Komba, amefunga rasmi hafla ya kuwaaga wajumbe 15 wanaotarajia kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia programu ya GGML Kili Challenge, inayofadhiliwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML).
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jana, Beda aliwataka watumishi wa umma na wananchi wa Mkoa wa Geita kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya magonjwa kwa kuzingatia afya zao, akisisitiza kuwa afya bora ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, aliwahimiza askari wa Jeshi la Polisi kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utekelezaji wa majukumu yao. Pia aliwasisitiza kuweka afya zao mbele ili kuongeza ufanisi na ubora wa utendaji kazi.

Naye Dkt. Omar Sukari alisema tukio hilo limewanufaisha wananchi wa Mkoa wa Geita kwa kuwapatia huduma za upimaji wa afya bila malipo, zikiwemo kupima makundi ya damu na kupata elimu kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza na kwamba hatua hiyo inasaidia kugundua na kudhibiti magonjwa mapema.

Shughuli hiyo ilijumuisha matembezi ya kuhamasisha afya kwa jamii, utoaji wa elimu ya afya pamoja na huduma za upimaji wa Virusi vya UKIMWI (VVU), ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kitaifa za kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI kupitia programu ya The Kili Challenge Initiatives.
Akihitimisha hafla hiyo, Kaimu Meneja Mkuu wa GGML, Duan Campbell, alilishukuru Jeshi la Polisi, viongozi wa serikali, watumishi wa taasisi mbalimbali na wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki Siku ya Afya Geita na hafla ya kuwaaga washiriki wa GGML Kili Challenge.

Alisema ushiriki wao unaonyesha dhamira ya pamoja ya kujenga jamii yenye afya bora na kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza ustawi wa wananchi wa Mkoa wa Geita.
Programu ya GGML Kili Challenge inalenga kuhamasisha jamii kuchukua hatua dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya afya kwa ujumla. Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya GGML vilivyopo Manispaa ya Geita, mkoani Geita.
Leave a comment