Na George Gabriel

Wananchi wa Kata ya Nanyumbu wamepongeza ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Magala, wakisema imeleta manufaa makubwa kwa jamii kupitia usikilizaji wa kero, utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na usimamizi wa ugawaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati.

Wakizungumza baada ya kukamilika kwa ziara hiyo, wananchi walisema hatua ya Mkuu wa Wilaya kufika moja kwa moja katika maeneo yao imeongeza imani kwa Serikali kwa kuwapa fursa ya kueleza changamoto zao na kupata ufumbuzi wa haraka.

Fatuma Abdalah alisema migogoro iliyokuwa ikiwakabili wakulima na wafugaji imeanza kutafutiwa ufumbuzi, jambo ambalo litasaidia kurejesha amani na kuongeza uzalishaji.

“Tunamshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutusikiliza. Migogoro iliyokuwa inatukabili kati ya wakulima na wafugaji imeanza kutafutiwa ufumbuzi, jambo litakalorejesha amani na kuongeza uzalishaji,” alisema Fatuma.

Naye Juma Shaibu alisema ziara hiyo imeonesha dhamira ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kwa vitendo badala ya kusubiri malalamiko yafikishwe ofisini.

“Tunafurahi kuona viongozi wanakuja vijijini kusikiliza matatizo yetu. Pia tunashukuru pembejeo za kilimo zimeanza kutolewa mapema, jambo litakalotusaidia kujiandaa vizuri kwa msimu wa kilimo,” alisema Juma.

Kwa upande wake, Shaiki Ulenje aliipongeza Serikali kwa juhudi za kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo kwa muda mrefu imekuwa chanzo cha migongano katika kata hiyo. Alisema maamuzi yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo yameleta matumaini mapya kwa wananchi.

“Tunampongeza Magala kwa kusimamia haki na kuhakikisha kila upande unasikilizwa. Tunayo imani kuwa amani itaendelea kudumu na shughuli za uzalishaji zitaimarika,” alisema Ulenje.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Magala, alisema ziara hiyo imelenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati, kufuatilia utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo, pamoja na kuhakikisha ugawaji wa pembejeo za kilimo unafanyika kwa uwazi na haki ili kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo.

Posted in

Leave a comment