
Na Jastini Bukebuke
Polisi Kata wa Ihanamilo, INSP Yosepha Michael, Julai 20, 2026, alitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyakahengele, Wilaya ya Geita, Mkoa wa Geita, akiwahimiza kuwa wazalendo, wenye nidhamu na bidii katika masomo ili kujijengea msingi imara wa maisha yao ya baadaye.
Akizungumza wakati wa elimu hiyo, INSP Michael alisema elimu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya mtu binafsi na taifa, hivyo aliwataka wanafunzi kuipenda shule, kuwaheshimu walimu na wazazi, pamoja na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha masomo na mustakabali wao.
Aidha, aliwakumbusha kuzingatia tahadhari za kiusalama kwa kujilinda dhidi ya vitendo vya kihalifu. Aliwashauri kutembea kwa makundi wanapokwenda na wanaporudi kutoka shuleni, kuepuka kuzungumza na watu wasiowafahamu, pamoja na kutoa taarifa kwa walimu, wazazi au Jeshi la Polisi wanapobaini viashiria vya uhalifu au mazingira yasiyo salama.
Kwa upande wao, wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyakahengele walilishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu hiyo, wakisema imewaongezea uelewa kuhusu umuhimu wa elimu, uzalendo na mbinu za kujilinda dhidi ya vitendo vya kihalifu.


Pia waliahidi kuendelea kushirikiana, kuishi kwa upendo, kuzingatia maadili mema na kufuata ushauri walioupata ili kuendelea kuwa salama wawapo shuleni na wanaporejea nyumbani.
Leave a comment