Na Damasi Kalembwe

Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Mabwepande, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, limetoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika Kituo cha Babu na Bibi Children’s Care kilichopo Madale, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano na jamii na kuwajali watoto wenye mahitaji maalumu.

Ziara hiyo ilifanyika juzi chini ya uongozi wa OCD Mabwepande, SSP Colle Mshauri, akifuatana na maofisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi, akiwemo OCS Madale, SP Ngoso, DTO Mabwepande, ASP Joseph, DFBO Mabwepande, ASP Elizabeth, I/C CID Madale, ASP Virgiana, pamoja na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Katika ziara hiyo, Jeshi la Polisi lilikabidhi msaada uliokuwa na fedha taslimu shilingi 100,000, unga, mchele, sukari, mafuta ya kula, pampasi na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaolelewa katika kituo hicho.

Akizungumza kwa niaba ya kituo hicho, mlezi wake, Diocres Apolnary Mutalemwa, alilishukuru Jeshi la Polisi kwa moyo wa kujitolea na kuwajali watoto wenye mahitaji maalumu.

Alisema msaada huo ni faraja kubwa na utasaidia kupunguza baadhi ya changamoto zinazokikabili kituo katika kuhudumia watoto.

Mutalemwa alibainisha kuwa ushirikishwaji wa jamii unaofanywa na Jeshi la Polisi unaendelea kuwa daraja muhimu la kuimarisha uhusiano kati ya polisi na wananchi, huku ukihamasisha mshikamano na uwajibikaji wa kijamii.

Kituo cha Babu na Bibi Children’s Care kinahudumia watoto 68 wa rika mbalimbali kuanzia miaka mitatu na kuendelea huku baadhi yao wanasoma katika vyuo, shule za sekondari, msingi na chekechea.

Msaada huo unatarajiwa kuboresha ustawi wa watoto hao na kuendeleza mshikamano kati ya Jeshi la Polisi na jamii.

Posted in

Leave a comment