Na George Gabriel

Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu imeendelea kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma kwa kuendesha vikao kazi maalum vinavyolenga kuongeza uelewa kuhusu maadili ya utumishi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Vikao hivyo vilivyoratibiwa na Idara ya Utumishi na Utawala vilifanyika kuanzia Julai 14 hadi 17, 2026 katika Tarafa za Maratani, Nanyumbu, Nakopi na Mangaka.

Lengo la vikao hivyo lilikuwa kuwajengea watumishi uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali, sambamba na kutoa fursa ya kusikiliza changamoto, maoni na mapendekezo yao ili kuboresha mazingira ya kazi na utoaji wa huduma.

Akizungumza wakati wa vikao hivyo, Afisa Tawala wa Wilaya ya Nanyumbu, Mebu Kalembo, aliwataka watumishi kuwa waadilifu, wawajibikaji na wenye nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Alisisitiza kuwa utendaji unaozingatia maadili ya utumishi wa umma ni msingi wa kuongeza ufanisi na kujenga imani ya wananchi kwa Serikali.

“Kila mtumishi anatakiwa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati,” alisema Kalembo.

Katika mafunzo hayo, washiriki walipatiwa elimu kuhusu maadili ya utumishi wa umma, haki na wajibu wa mtumishi, mamlaka za kinidhamu, itifaki na ustaarabu mahali pa kazi, mawasiliano serikalini pamoja na matumizi ya Mfumo wa Kielektroni wa Kupokea Malalamiko, Ushauri na Pongezi (e-Mrejesho).

Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Maulid Chidoli, aliwasilisha mada kuhusu Mfumo wa Kielektroni wa Tathmini ya Utendaji wa Watumishi wa Umma (PEPMIS), akieleza kuwa mfumo huo unasaidia kupima utendaji wa watumishi kwa uwazi, kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, aliwakumbusha watumishi kutumia mfumo huo ipasavyo kwa kuzingatia malengo ya kazi, huku akiwahimiza kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, ikiwemo mikopo inayoratibiwa kupitia Hazina, kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Washiriki wa vikao hivyo walieleza kuwa mafunzo hayo yamewaongezea uelewa kuhusu wajibu wao, matumizi sahihi ya mifumo ya Serikali na mbinu za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hatua hiyo inaakisi dhamira ya Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu ya kuendelea kujenga utumishi wenye maadili, uwajibikaji na ufanisi, sambamba na kutekeleza azma ya Serikali ya kuboresha huduma za umma kwa manufaa ya wananchi wote.

Posted in

Leave a comment