Na Damasi Kalembwe

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni limewataka wamiliki wote wa vyombo vya moto kujitokeza kuhakiki magari yao na kuzingatia taratibu za usalama barabarani, likisisitiza kuwa kampeni ya “Nenda kwa Usalama” inalenga kupunguza ajali na kulinda maisha ya watumiaji wote wa barabara.

Zoezi hilo linafanyika katika Kituo cha Polisi Oysterbay cha Zamani kuanzia Julai 23, 2026, chini ya usimamizi wa Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, SSP Adamson Mwangamilo.

Sambamba na zoezi hilo, wananchi wanaendelea kupatiwa elimu kuhusu matumizi salama ya vyombo vya usafiri, ikiwemo magari na pikipiki, pamoja na namna ya kujaza taarifa katika mfumo wa ukaguzi wa magari ili kupata stika za MIMIS.

Hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuimarisha usalama barabarani.

Miongoni mwa wananchi walioshiriki katika zoezi hilo ni Shabani Omary, ambaye amelipongeza Jeshi la Polisi pamoja na Serikali kwa kuanzisha mfumo wa kisasa wa ukaguzi wa magari.

Amesema mfumo huo umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa kupunguza muda wa kusubiri na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kinaendelea na zoezi la uhakiki wa magari na utoaji wa stika za “Nenda kwa Usalama” ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuimarisha usalama barabarani na kuhamasisha uzingatiaji wa sheria za usalama wa barabarani.

Posted in

Leave a comment