
Na George Gabriel
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, ameridhishwa na maandalizi yanayofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu kuelekea Maonesho ya Nanenane 2026, huku akisisitiza kuwa kazi zilizobaki zikamilishwe kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Kanali Msengi alitoa kauli hiyo jana baada ya kukagua banda la Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, ambapo alipongeza hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya maonesho hayo.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Ibrahim Mwanauta, alisema halmashauri imejipanga kikamilifu kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ili kuhakikisha banda la Nanyumbu linakuwa miongoni mwa mabanda bora katika Maonesho ya Nanenane 2026.
Mwanauta aliwataka wakuu wote wa idara na vitengo kushiriki kikamilifu katika maandalizi hayo, hususan maafisa wa kilimo, mifugo na biashara, kwa kuandaa maonesho yatakayoonesha ubunifu, matumizi ya teknolojia na mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema maonesho hayo ni fursa muhimu ya kuitangaza Wilaya ya Nanyumbu, kuvutia wawekezaji, kutoa elimu kwa wananchi na kuonesha huduma mbalimbali zinazotolewa na halmashauri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Magala, amewasihi wananchi wa wilaya hiyo na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya Nanenane 2026 yatakayofanyika katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.
Alisema maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kujifunza teknolojia za kisasa katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na biashara, pamoja na kupata fursa za masoko na uwekezaji zitakazochangia kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Maonesho ya Nanenane 2026 Kanda ya Kusini yanatarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026, katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
Serikali imeendelea kuwahimiza wananchi kutumia maonesho hayo kama fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mpya ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuchochea maendeleo ya uchumi.


Leave a comment