Na Andrea Mlwafu

Kuna mtu anayeandika wimbo akiwa chumbani kwake, mwingine anashona vazi linalogeuka kuwa mtindo unaotafutwa na wengi, mwingine anachora picha, anapiga video, anatengeneza filamu au anaunda maudhui kwa kutumia simu yake.

Kazi zao zinaweza kuonekana kama vipaji vya kawaida mpaka pale zinapowafikia watu wengi na kuanza kuzalisha fedha. Lakini nyuma ya kila wimbo, filamu, picha, video au ubunifu mwingine kuna swali ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiwasumbua wabunifu wengi Tanzania: Kipaji kinawezaje kugeuzwa kuwa mali inayozalisha kipato endelevu?

Swali hilo sasa linaingia kwenye mjadala mpana zaidi kuhusu uchumi wa ubunifu nchini.

Katika Mkutano wa Uchumi wa Ubunifu wa MELACHA uliofanyika Dar es Salaam Septemba 2026, wadau walitaka mabadiliko katika mifumo ya upatikanaji wa fedha, bima, ulinzi wa hakimiliki na kodi, wakisema baadhi ya mifumo iliyopo haikuundwa kwa kuzingatia namna sekta ya ubunifu inavyofanya kazi.

Kwao, tatizo si ukosefu wa vipaji, bali ni mazingira yanayomzuia mbunifu kugeuza kipaji chake kuwa biashara inayoweza kukua na kuajiri wengine.

Kipaji Kinapotoka Chumbani na Kuingia Sokoni

Kwa muda mrefu, msanii wa Tanzania amekuwa akitazamwa zaidi kupitia kazi anayofanya kuliko thamani ya kiuchumi ya kazi hiyo. Mwanamuziki anaonekana kupitia wimbo wake, mwigizaji kupitia filamu, mpiga picha kupitia picha na mbunifu kupitia kazi yake.

Lakini katika uchumi wa kisasa wa ubunifu, kazi hiyo yenyewe inaweza kuwa mali yenye thamani, inayoweza kuuzwa, kupewa leseni, kutumika kibiashara na kuzalisha mapato kwa muda mrefu.

Hapo ndipo dhana ya hakimiliki inapokuwa muhimu.

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) inaeleza kuwa hakimiliki humpa mwandishi au mbunifu haki za kipekee juu ya kazi yake, zikiwemo haki za kuizalisha, kuichapisha, kuiwasilisha hadharani, kuitangaza na kuisambaza.

Kwa maana hiyo, wimbo, filamu, maandishi, picha, mchoro au kazi nyingine ya ubunifu si kitu cha kuposti na kusahaulika tu; inaweza kuwa mali ya mwenye kuibuni.

Naomi Mungure, Kaimu Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki wa COSOTA, amekuwa sehemu ya mijadala ya kimataifa kuhusu namna mifumo ya hakimiliki inavyopaswa kubadilika kutokana na teknolojia mpya, ikiwemo akili bandia.

Katika mkutano wa CISAC uliofanyika Paris mwaka huu, COSOTA ilishiriki majadiliano kuhusu usajili na uthibitishaji wa kazi, ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha pamoja na changamoto mpya zinazoletwa na akili bandia katika kazi za ubunifu.

Hakimiliki Isipokuwa Fedha, Inabaki Karatasi

Changamoto mojawapo inayojitokeza kwenye sekta ya ubunifu ni tofauti kati ya kuwa na haki kwenye karatasi na kuwa na uwezo wa kuzitumia haki hizo kupata fedha.

Msanii anaweza kuwa ametengeneza kazi yake, lakini ikiwa kazi hiyo inasambazwa, inatumika kibiashara au kunakiliwa bila utaratibu unaompa mwenye kazi sehemu ya mapato, thamani yake inaweza kupotea.

Ndiyo maana usajili wa kazi na uelewa wa mikataba ni muhimu.

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) inaeleza kuwa wabunifu wanaweza kusajili kazi mbalimbali kama muziki, filamu, picha, maandishi, maigizo na kazi nyingine za ubunifu, huku taasisi hiyo ikiwa na jukumu pia la kuwezesha wenye haki kudai na kupokea mirabaha.

Hii inaweka mbele changamoto nyingine: mbunifu anahitaji kujua si tu namna ya kutengeneza kazi nzuri, bali pia namna ya kuimiliki.

Katika dunia ambayo wimbo unaweza kutumika kwenye tangazo, picha ikaingia kwenye kampeni ya kampuni, video ikawa sehemu ya jukwaa la kidijitali au filamu ikaonyeshwa katika nchi nyingine, kutokujua thamani ya haki zako kunaweza kumfanya mbunifu apoteze mapato ambayo hakuwahi kuyajua.

Fedha Zinapotafuta Vipaji

Changamoto nyingine kubwa imekuwa mtaji.

Kamera, kompyuta, vifaa vya kurekodia, programu za kuhariri, studio, usafiri na gharama za uzalishaji vinahitaji fedha. Wakati mwingine kipaji kipo, lakini vifaa vya kukiwezesha kukua havipo.

Mwaka 2026, Serikali ilitangaza uwezeshaji wa watengeneza maudhui mtandaoni kupitia fedha zilizotengwa kwa ajili ya sekta ya ubunifu.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alisema Sh bilioni 2 zimetolewa kama mikopo kwa watengeneza maudhui, ndani ya Sh bilioni 20 zilizotengwa kwa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa.

Fedha hizo zililenga kusaidia watengeneza maudhui kupata vifaa, kuboresha uzalishaji na kuongeza uwezo wao wa kushindana katika soko la kidijitali.

Kwa mtazamo huo, Serikali inaanza kuiona kamera, kompyuta, vifaa vya uzalishaji na maudhui yenyewe kama sehemu ya uchumi unaoweza kuhitaji uwekezaji, badala ya kuutazama ubunifu kama burudani pekee.

Hata hivyo, fedha pekee haziwezi kujenga sekta.

Mbunifu akipewa mtaji bila elimu ya biashara, usimamizi wa fedha, masoko, hakimiliki na namna ya kutafuta masoko mapya, kuna hatari ya fedha kuishia kwenye uzalishaji wa kazi moja bila kujenga biashara endelevu.

Mwekezaji Anapomtazama Msanii Kama Mali

Katika ulimwengu wa biashara, mwekezaji haangalii tu kama mtu ana kipaji. Anaangalia kama kipaji hicho kinaweza kuzalisha thamani, kina soko na kinaweza kukua.

Hii ndiyo changamoto ambayo wadau wa sekta ya ubunifu waliibua katika MELACHA Creative Economy Summit 2026.

Khalila Mbowe, Mkurugenzi wa MELACHA, alisema mifumo mingi iliyopo haikubuniwa kwa kuzingatia mazingira ya watu wanaofanya kazi katika sekta ya ubunifu, ambao mapato yao mara nyingi hayafuati mfumo wa kawaida wa ajira yenye mshahara wa kila mwezi.

Kauli hiyo inaingia moja kwa moja kwenye suala la bima, mikopo na huduma za kifedha.

Mfanyakazi mwenye mshahara wa kila mwezi anaweza kuonyesha mapato yake kwa njia rahisi zaidi, lakini msanii anaweza kupata fedha nyingi mwezi mmoja na kukaa miezi kadhaa bila mradi mkubwa.

Hata hivyo, kutokuwa na mshahara wa kila mwezi hakumaanishi hana biashara.

Tatizo ni namna taasisi za fedha zinavyoweza kuitambua biashara hiyo.

Ikiwa wimbo unaingiza mirabaha, YouTube inalipa, kampuni zinaingia kwenye mikataba ya matangazo na kazi za ubunifu zinauzwa kwa wateja mbalimbali, basi kuna thamani ya kifedha inayoweza kuonekana, lakini inahitaji mifumo inayoweza kuipima.

Simu Inapogeuza Mtu Kuwa Kampuni

Miaka michache iliyopita, mtu aliyetaka kuingia kwenye uzalishaji wa maudhui alihitaji vifaa vya gharama kubwa na mara nyingi alitegemea kampuni au studio.

Leo, simu inaweza kuwa kamera, studio, chumba cha kuhariri na njia ya kusambaza kazi kwa hadhira ya ndani na nje ya Tanzania.

Mabadiliko hayo yamepanua mlango wa ubunifu.

Majukwaa ya kidijitali kama TikTok, YouTube, Instagram na mengine yamewapa wabunifu nafasi ya kujenga hadhira bila kusubiri kwanza kupata nafasi kwenye televisheni au redio.

Taarifa ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuhusu uchumi wa watengeneza maudhui inaonyesha kuwa majukwaa hayo yamekuwa sehemu muhimu ya mapato kwa watengeneza maudhui, huku pia kukiwa na changamoto za upatikanaji wa mifumo ya kimataifa ya uchumaji wa maudhui na malipo.

Hapo ndipo mbunifu wa leo anapobadilika na kuwa mjasiriamali wa kidijitali.

Anaweza kuwa mwandishi, mpiga picha, mhariri wa video, mtangazaji na msambazaji wa kazi yake kwa wakati mmoja.

Lakini kadiri fursa zinavyoongezeka, ndivyo ushindani unavyoongezeka.

Soko halihitaji tu mtu anayejua kutengeneza maudhui; linahitaji mtu anayejua kujenga chapa, kuelewa hadhira, kutunza haki zake na kutengeneza mfumo wa mapato.

Akili Bandia Inapogonga Mlango

Wakati Tanzania ikijifunza namna ya kujenga uchumi wa ubunifu wa kidijitali, teknolojia nyingine imeingia kwa kasi—akili bandia.

AI inaweza kusaidia kutengeneza picha, video, sauti, maandishi na hata muziki kwa muda mfupi.

Kwa upande mmoja, teknolojia hii inaweza kumpa mbunifu zana mpya za kuongeza kasi ya kazi na kujaribu mawazo ambayo hapo awali yalihitaji timu kubwa na fedha nyingi.

Kwa upande mwingine, inaleta maswali magumu kuhusu nani anamiliki kazi iliyotengenezwa kwa msaada wa AI, namna kazi za wasanii zinavyotumika kufundisha mifumo hiyo na jinsi mapato yanavyopaswa kugawanywa.

Mijadala ya COSOTA na taasisi nyingine za hakimiliki Afrika mwaka huu imeonesha kwamba suala hilo tayari limeingia kwenye ajenda ya ulinzi wa kazi za ubunifu.

Mijadala hiyo imehusisha pia mifumo ya usajili, uthibitishaji wa kazi na namna taasisi za hakimiliki zinavyoweza kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Kwa Tanzania, hili lina maana kwamba sheria na mifumo ya hakimiliki haitakiwi kuangalia tu namna wimbo au filamu inavyotengenezwa leo, bali inahitaji kujiandaa kwa mazingira ambayo mwanadamu na mashine wanaweza kushirikiana katika kutengeneza kazi.

Ubunifu Unapovuka Nje ya Tanzania

Kazi ya ubunifu, kama bidhaa nyingine, soko lake halipaswi kuishia ndani ya mipaka ya nchi.

Wimbo wa Kiswahili unaweza kusikilizwa Nairobi, Kigali au Johannesburg. Filamu inaweza kuuzwa kwenye jukwaa la kimataifa. Mchoro unaweza kutumiwa katika kampeni ya kampuni ya nje. Mavazi yanaweza kuingia kwenye soko la kimataifa.

Ndiyo maana Mpango wa Muda Mrefu wa Tanzania wa 2026/27–2050/51 umeweka malengo yanayohusisha kutumia majukwaa ya kidijitali kupanua ufikiaji wa wabunifu wa Tanzania, kujenga ushirikiano kati ya wabunifu na wataalamu wa teknolojia, kuimarisha ulinzi wa hakimiliki kwa watengeneza maudhui wa kidijitali na kuongeza uuzaji wa kazi za ubunifu za Tanzania kimataifa kupitia leseni za hakimiliki na mirabaha.

Hii ni hatua muhimu kwa sababu soko la kimataifa linahitaji zaidi ya kipaji.

Linahitaji viwango, mikataba, mifumo ya malipo, ulinzi wa haki, mawakala, wasimamizi wa kazi na uwezo wa kujenga chapa inayotambulika.

Bila miundombinu hiyo, kazi inaweza kuwafikia watu wengi lakini mapato yakabaki madogo.

Kutoka Maonyesho Hadi Soko la Haki za Ubunifu

Mwelekeo mpya unaonekana pia kwenye Maonyesho ya Mashariki Creative Economy Expo 2026 yaliyofanyika Dar es Salaam, ambayo yamejenga dhana ya kuunganisha wabunifu, wanunuzi, wawekezaji na taasisi ili kazi za ubunifu zionekane kama mali inayoweza kuuzwa na kuwekewa uwekezaji.

Maonyesho hayo yameweka mkazo kwenye biashara ya haki za kazi za ubunifu, ikiwemo haki za filamu, ubia wa uzalishaji na mifumo ya mirabaha kwa wabunifu.

Hapa ndipo tasnia inaweza kuanza kuondoka kwenye utamaduni wa kumsubiri msanii awe maarufu ndipo kampuni zimtafute.

Badala yake, kazi yenyewe inaweza kuanza kuwa na thamani hata kabla jina la mbunifu halijawa kubwa.

Mwekezaji anaweza kuangalia haki za filamu, kampuni ikaangalia matumizi ya wimbo, hoteli ikaangalia kazi za sanaa za mapambo, jukwaa likaangalia maudhui na taasisi ikaangalia ubia wa uzalishaji.

Kwa mtazamo huo, ubunifu unaweza kuwa soko lenye bidhaa nyingi tofauti, si sekta inayotegemea mtu mmoja kuwa maarufu.

Tatizo Haliishii Kwenye Kutengeneza Kazi

Kuna wakati msanii anaweza kutumia miezi kutengeneza kazi ambayo mtu mwingine anaweza kuichukua kwa sekunde chache na kuiweka kwenye ukurasa wake.

Picha inaweza kunakiliwa, video ikawekwa tena, wimbo ukasambazwa bila utaratibu au kazi ikatumika kibiashara bila mwenyewe kujua.

Changamoto kama hizi zinaonyesha kwa nini elimu ya hakimiliki inahitaji kwenda sambamba na ukuaji wa teknolojia.

Utafiti kuhusu ulinzi wa hakimiliki Tanzania katika zama za kidijitali umeonyesha changamoto zinazohusisha usimamizi wa haki za kidijitali, unakili usioidhinishwa na usambazaji wa kazi mtandaoni.

Kwa hiyo, mbunifu wa kizazi kipya anahitaji kuwa na ujuzi wa aina mbili.

Anahitaji kujua namna ya kutengeneza kazi inayovutia, lakini pia ajue namna ya kuilinda na kuifanya izalishe fedha.

Hapo ndipo kipaji kinapogeuka taaluma na taaluma inapogeuka biashara.

Tanzania Inatakiwa Kujenga Mfumo, Si Matukio Pekee

Mikutano, maonyesho, mikopo na programu za uwezeshaji zinaweza kuwa mwanzo mzuri, lakini sekta ya ubunifu haiwezi kujengwa kwa matukio ya mara moja.

Inahitaji mfumo unaoendelea kufanya kazi hata baada ya kamera za uzinduzi kuzimwa.

Mfumo huo unahitaji taasisi za fedha kuelewa biashara za wabunifu, bima zinazoweza kuwahudumia watu wenye mapato yasiyo ya mshahara wa kila mwezi, sheria zinazolinda kazi katika mazingira ya kidijitali, mifumo madhubuti ya ukusanyaji wa mirabaha, elimu ya biashara kwa wabunifu na masoko yanayowaunganisha wenye kazi na wanunuzi.

Khalila Mbowe anasema kuna umuhimu wa kufanya sekta ya ubunifu iweze kuvutia uwekezaji na kuzalisha biashara na ajira endelevu.

Hoja hiyo inafanya mjadala uondoke kwenye swali la, “Tuwasaidie wasanii?” na kuelekea kwenye swali pana zaidi: “Tunawezaje kujenga mazingira ambayo msanii anaweza kujenga biashara yake mwenyewe?”

Kipaji Kisipotelee Njiani

Tanzania haina tatizo la kukosa watu wenye uwezo wa kuimba, kuandika, kuchora, kuigiza, kupiga picha, kutengeneza filamu, kubuni mavazi au kuunda maudhui.

Changamoto kubwa ni kuhakikisha uwezo huo hauishii kwenye makofi ya hadhira pekee.

Kipaji kinapopata mtaji kinaweza kuzalisha kazi.

Kazi inapolindwa na hakimiliki inaweza kuwa mali.

Mali inapopata soko inaweza kuleta mapato.

Mapato yanapowekezwa tena yanaweza kujenga biashara.

Na biashara inapokua, inaweza kuajiri watu wengine na kuleta thamani kwenye uchumi.

Hapo ndipo maana halisi ya uchumi wa ubunifu inapoonekana.

Si kwamba Tanzania inataka wasanii watengeneze kazi nyingi zaidi. Inataka pia kazi hizo ziwe na thamani, zilindwe, ziuzwe na ziweze kumrudishia mbunifu kipato cha muda mrefu.

Kwa sababu mwisho wa yote, kipaji kisipokuwa na mfumo wa kukilinda na kukiendeleza kinaweza kubaki kuwa kipaji tu.

Lakini kipaji kinapounganishwa na biashara, teknolojia, hakimiliki, mtaji na soko, kinaweza kubadilika na kuwa mali yenye thamani.

Na hapo ndipo Tanzania inapokabiliwa na jukumu jipya: si kutafuta vipaji pekee, bali kujenga uchumi unaojua thamani ya vipaji ilivyo navyo.

Posted in

Leave a comment