Na Pilastus Nyaulingo

Abiria wanaotumia Kituo cha Mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam wamelalamikia upungufu wa maeneo ya kukaa na msongamano katika vyoo, wakisema hali hiyo inawalazimu baadhi yao kusimama kwa muda mrefu au kukaa juu ya mizigo wakati wakisubiri mabasi yao.

Malalamiko hayo yameibuka siku chache baada ya kituo hicho kuanza kupokea kwa wingi abiria wanaopanda na kushuka kituoni hapo, kufuatia maelekezo ya Serikali ya kusitisha shughuli hizo katikati ya jiji.

Tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kuagiza mabasi kurejea ndani ya kituo hicho, idadi ya abiria imeongezeka na kuongeza shinikizo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kusubiri.

Richard Malima, abiria wa basi la kwenda Kyela mkoani Mbeya, alisema upungufu wa viti na maeneo ya kusubiri unapaswa kupewa kipaumbele kwa sababu baadhi ya abiria hutumia muda mrefu kituoni kabla ya safari zao.

“Ingawa upungufu wa viti unaweza kuonekana kama changamoto ndogo, kituo kinachohudumia maelfu ya wasafiri kila siku kinapokosa maeneo ya kutosha ya kusubiri kinaweza kuathiri ubora wa huduma na ustawi wa abiria,” alisema Malima.

Alishauri Serikali na uongozi wa kituo kuangalia uwezekano wa kuongeza maeneo maalumu ya kusubiri ili abiria waweze kukaa kwa usalama wakati wakisubiri safari zao.

Linna Siya, abiria wa basi la kwenda Kanda ya Ziwa, amesema mazingira ya kusubiri yanahitaji kuboreshwa, hasa kwa abiria wanaotumia muda mrefu kituoni.

Amesema baadhi ya abiria huambiwa kwenda ghorofani kusubiri, lakini wengine huamua kubaki chini karibu na mabasi kwa hofu ya kuyakosa yanapokuwa tayari kuondoka.

“Unapofika hapa, mazingira yanachosha. Unaenda juu kununua tiketi, lakini hakuna sehemu ya kukaa katika ofisi hizo. Tunaambiwa tushuke chini na kusubiri hadi muda wa basi kuondoka,” alisema Siya.

Alisema hali hiyo inaweza kuwa ngumu zaidi kwa wazee, wanawake wajawazito, watoto na watu wenye mahitaji maalumu ambao wanaweza kushindwa kusimama au kukaa juu ya mizigo kwa muda mrefu.

Abiria mwingine, Omary Mohamed, alipendekeza kuwekwa kwa viti katika eneo la chini karibu na maegesho ya mabasi ili abiria waweze kusubiri bila kulazimika kwenda ghorofa ya juu.

“Ushauri wangu ni kuweka viti huku chini. Kuna nafasi na watu wanaweza kusubiri badala ya kusimama kwa muda mrefu,” alisema Mohamed.

Kituo hicho kina eneo maalumu la kusubiri abiria lililopo ghorofa ya kwanza. Hata hivyo, baadhi ya abiria wamesema hawapendi kutumia eneo hilo kwa sababu liko mbali na sehemu ambazo mabasi huegeshwa.

Uchunguzi uliofanywa kituoni hapo, ulibaini kuwa eneo la kusubiri linatumika kwa shughuli mbalimbali za biashara, ikiwemo uuzaji wa nguo na vitabu, huduma za kuchaji simu na uuzaji wa chakula, hali inayopunguza nafasi inayopatikana kwa abiria wakati kituo kinapokuwa na msongamano.

Abiria pia wamelalamikia malipo ya Sh300 wanapohitaji kutoka katika eneo la kusubiri, licha ya kuwa tayari wamelipa gharama nyingine wanapoingia kituoni.

Kaimu Meneja wa Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Naamini Nguve, alisema kituo kina eneo maalumu la kusubiri lililopo ghorofa ya kwanza na kwamba lina uwezo wa kuhudumia abiria.

Alisema eneo hilo lina sehemu tatu na limewekewa televisheni, likiwawezesha abiria kupata sehemu ya kukaa na kujisitiri wakati wakisubiri mabasi yao.

Kuhusu pendekezo la kuweka viti katika eneo la chini karibu na mabasi, Nguve alisema hatua hiyo inaweza kuleta changamoto kutokana na mpangilio wa kituo na maeneo yaliyotengwa kwa wafanyabiashara.

Alisema kuweka viti katika eneo hilo kunaweza kusababisha mgongano wa matumizi ya nafasi kati ya abiria na wafanyabiashara waliokodi maeneo hayo.

Kuhusu lifti isiyofanya kazi, Nguve alisema uongozi unaendelea na maboresho ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ufanisi na kwa wakati kulingana na mahitaji ya kituo.

Mbali na changamoto ya maeneo ya kusubiri, abiria na watu wanaofanya kazi kituoni hapo pia wamelalamikia msongamano katika vyoo.

Juma Abdallah, mpagazi anayefanya kazi katika kituo hicho, amesema ongezeko la abiria limeongeza mahitaji ya huduma za vyoo.

“Nimekuwa nikifanya kazi hapa nikibeba mizigo tangu jana. Kuna msongamano mkubwa kwenye vyoo na unalazimika kupanga foleni ili kupata huduma,” alisema Abdallah.

Kwa upande wake, Johnson Peter amesema foleni wakati mwingine huongezwa na baadhi ya watu wanaotumia muda mrefu ndani ya vyoo licha ya kujua kuwa kuna watu wengine wanasubiri nje.

“Unajua, baadhi ya watu huchukua muda mrefu ndani hata wanajua kuna watu wengi wanasubiri,” alisema Peter.

Hata hivyo, Nguve alisema kituo kina vyoo vya kutosha na vya kisasa vinavyohudumia makundi mbalimbali, wakiwemo watu wenye mahitaji maalumu.

Amesema kituo kina jumla ya vitalu 18 vya vyoo vyenye zaidi ya vyumba 140, lakini changamoto iliyopo ni baadhi ya abiria kutofahamu maeneo vilipo.

Nguve alisema uongozi utaanza kutoa matangazo kwa abiria ili kuwaelekeza maeneo yenye vyoo na kuwasaidia kutumia huduma hizo kwa ufanisi.

Ongezeko la abiria katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli limekuja baada ya Serikali kuelekeza mabasi yanayofanya safari za mikoani kusitisha kupakia na kushusha abiria katikati ya jiji, hatua iliyofanya kituo hicho kuwa na shughuli nyingi zaidi.

Hali hiyo imeongeza umuhimu wa kuhakikisha maeneo ya kusubiri, vyoo, lifti na huduma nyingine muhimu zinaendana na idadi ya abiria wanaotumia kituo hicho.

Kwa abiria, changamoto kubwa ni kupata mazingira salama na yenye heshima wakati wakisubiri safari zao, huku uongozi wa kituo ukisisitiza kuwa baadhi ya huduma zipo lakini zinahitaji abiria kuelekezwa vizuri kuhusu maeneo zinakopatikana.

Posted in

Leave a comment