Na Pilastus Nyaulingo

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka taasisi za elimu kuhakikisha ubora wa elimu nchini unaendelea kuzingatiwa, akionya dhidi ya mfumo unaoweza kuwafanya wanafunzi kupata alama kubwa bila kuwa na uwezo na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Dkt. Nchemba alitoa kauli hiyo leo wakati akifunga Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mkoani Tanga, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wahitimu wanakuwa na uwezo halisi wa kutekeleza majukumu yao katika maeneo waliyosomea.

Alisema taasisi zinazohusika na uhakiki wa ubora wa elimu zinapaswa kuhakikisha viwango vinaendelea kuzingatiwa ili elimu inayotolewa nchini iwe na tija kwa mwanafunzi na Taifa kwa ujumla.

“Tusitengeneze mazingira ambayo kusoma kunakuwa rahisi na alama zinakuwa kubwa sana, halafu wahitimu wanapofika kazini wanapata sifuri kubwa. Hilo halikubaliki,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema ubora wa mafunzo ni muhimu zaidi katika sekta zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, zikiwemo afya, uhandisi na elimu, kwa kuwa Taifa linahitaji wataalamu wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa usahihi.

“Hatuwezi kucheza kamari na afya za Watanzania kwa kuwafundisha wataalamu vibaya halafu tukatarajia matokeo mazuri. Tunahitaji walimu na wahandisi wenye uwezo; wanapojenga daraja au jengo, ni lazima liwe salama na lenye ubora,” alisema Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu imekuwa sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika kuimarisha elimu inayounganisha nadharia na ujuzi wa vitendo.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi na umahiri unaowawezesha kujiajiri na pia kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi zake kuhakikisha ubunifu unaofanywa na Watanzania hauishii kwenye maonesho, bali unaendelezwa hadi kufikia uzalishaji na kuuzwa sokoni.

Alisema Tanzania ina wabunifu wenye uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali, lakini changamoto iliyopo ni kuhakikisha mawazo na bidhaa zao zinalindwa, zinaendelezwa na hatimaye kutumika katika maisha halisi.

“Ni lazima tuondoke kwenye maonesho na kwenda kwenye maisha halisi, kuhakikisha kinachooneshwa kwenye matukio kama haya kinakuwa sehemu ya maisha ya kila siku na kinaingia sokoni,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika sayansi, ujuzi na ubunifu kwa kuwa maeneo hayo ni muhimu katika kuibadilisha uchumi wa Taifa na kuongeza kasi ya maendeleo kupitia matumizi ya tafiti na teknolojia.

“Hatutaweza kuendelea bila sayansi, teknolojia na utafiti na bila kutumia matokeo ya tafiti hizo. Hatuwezi kuongeza uzalishaji bila kutumia matokeo ya utafiti,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameitaka mipango ya maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Tanga kuzingatia mahitaji ya kiuchumi na kijamii ya mkoa huo kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

Alisema miundombinu inayojengwa sasa inapaswa kuandaliwa kwa kuzingatia ongezeko la biashara, uwekezaji na usafiri wa anga katika siku zijazo, akieleza kuwa Tanga ina nafasi muhimu kama lango la kiuchumi kutokana na miradi mikubwa inayotekelezwa mkoani humo.

Posted in

Leave a comment