
Na Jastini Bukebuke, Geita
Mwanamke maarufu kwa jina la Mwinjilisti amewashangaza washiriki wa uzinduzi wa Geita Polisi Jamii Jogging Club uliofanyika jana katika Uwanja wa Kalangalala, Manispaa ya Geita, baada ya kushiriki kikamilifu katika mazoezi ya jogging licha ya umri wake mkubwa.
Ushiriki wake ulimvutia Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, ambaye alimpongeza na kumtia moyo kwa kumkabidhi vifaa vya michezo pamoja na fedha kama motisha, akimtambua kwa moyo wake wa dhati wa kuunga mkono michezo, afya na ustawi wa jamii.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, pia alimpongeza Mwinjilisti kwa kuwa mfano bora wa ushiriki wa jamii katika shughuli za michezo na afya.
SACP Jongo alisisitiza umuhimu wa wananchi kutoka makundi na rika mbalimbali kushiriki katika shughuli za michezo, akieleza kuwa ushiriki wa jamii katika michezo husaidia kuimarisha afya, mshikamano na mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Uzinduzi wa Geita Polisi Jamii Jogging Club umeendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kujenga jamii yenye afya, mshikamano na usalama.
Ushiriki wa Mwinjilisti ulikuwa miongoni mwa vivutio vya uzinduzi huo, ukitoa somo kwamba umri si kikwazo katika kushiriki shughuli za kuimarisha afya na ustawi wa jamii.
Mwinjilisti alionesha ustahimilivu wa hali ya juu wakati wa mazoezi hayo na kufanikiwa kuyamaliza bila kuonesha dalili za kuchoka, jambo lililowavutia na kuwapa hamasa washiriki wengine.

Leave a comment