
Na George Gabriel
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Edward Magala, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wilayani humo kubuni na kutekeleza miradi itakayowawezesha kujitegemea kifedha badala ya kutegemea fedha za wafadhili pekee.
Magala alitoa wito huo hivi karibuni wakati akifungua Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu.
Alisema ni muhimu kwa mashirika hayo kujenga uwezo wa kutekeleza miradi kwa ufanisi na weledi, huku yakizingatia maadili, misingi na vipaumbele vya jamii.
Magala alionya kuwa utegemezi mkubwa wa fedha za wafadhili unaweza kuhatarisha mwendelezo wa miradi endapo ufadhili huo utakoma. Hivyo, alizitaka NGOs kubuni vyanzo mbadala vya mapato na kuimarisha ubunifu ili ziweze kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uendelevu.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Anyesi John Mhalu alipongeza hatua ya Serikali ya kuwakutanisha wadau hao, akisema jukwaa hilo ni muhimu katika kujenga uwezo, kubadilishana uzoefu na kujadili namna bora ya kuboresha utendaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Rudrick Charles, alisema Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali huratibiwa kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO).
Alisema kupitia jukwaa hilo, mashirika huwasilisha na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli na miradi yao, pamoja na kubainisha changamoto na fursa zinazohusu utendaji wao.
Jukwaa hilo lilishirikisha pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na mashirika saba yasiyo ya kiserikali yanayotekeleza shughuli mbalimbali katika Wilaya ya Nanyumbu.
Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2026 limebebwa na kaulimbiu: “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani.”

Leave a comment