Na Mwandishi Wetu, Nachingwea – Lindi

Wajasiriamali wa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, wametakiwa kutumia kwa ufanisi mitaji wanayopewa na Halmashauri ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Bi. Stella Kategile, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajasiriamali kutoka vikundi mbalimbali yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mondulane Messi.

Kategile alisema matumizi sahihi ya mitaji yatawawezesha wajasiriamali kufikia malengo waliyojiwekea na kukuza biashara na shughuli zao za kiuchumi, badala ya kutumia fedha hizo kwa mambo tofauti na mpango waliouwasilisha na kuidhinishiwa.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii, James Mbakile, alisema wajasiriamali wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli zao, zikiwemo utoaji na usimamizi wa mitaji, usimamizi wa mapato na matumizi, ukosefu wa masoko, teknolojia pamoja na mabadiliko ya mazingira ya kibiashara.

Naye Mkaguzi wa Ndani, Mesia Mlay, aliwataka wanachama wa vikundi kutunza kumbukumbu sahihi za fedha ili kuhakikisha uwazi na ufanisi katika uendeshaji wa shughuli zao.

Alisema kutokuwepo kwa kumbukumbu sahihi kunasababisha changamoto mbalimbali, ikiwemo wanakikundi kushindwa kufahamu kiwango halisi cha fedha kinachoingia, kupotea kwa uaminifu miongoni mwa wanachama, pamoja na kushindwa kubaini kiasi cha fedha kinachodaiwa na kinachodaiwa na wengine.

Aidha, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Aurelia Haule, alieleza umuhimu wa vikundi vya wajasiriamali kujenga utamaduni wa kuweka akiba.

Alisema akiba husaidia vikundi kukabiliana na dharura, kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuongeza uwekezaji, kujenga umoja na ushirika miongoni mwa wanachama, kutumia fursa za biashara kwa wakati na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha.

Kwa upande wake, Afisa Sheria, Diana Mmary, alisema ukosefu wa mawasiliano thabiti miongoni mwa wanakikundi ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya migogoro inayoweza kudhoofisha maendeleo ya vikundi.

Alisema hali hiyo inaweza kusababisha baadhi ya wanachama kujiondoa katika vikundi na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa malengo na mipango ya maendeleo.

Mafunzo hayo yamehusisha zaidi ya vikundi 20 vya wajasiriamali pamoja na maafisa kutoka idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, kwa lengo la kuwajengea uwezo katika usimamizi wa mitaji, fedha, kumbukumbu za kifedha, biashara na utatuzi wa changamoto zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa vikundi.

Posted in

Leave a comment