
Na Pilastus Nyaulingo
Katika jamii nyingi, mwanaume hukua akifundishwa kuwa imara, kuvumilia changamoto na kutokuonyesha udhaifu mbele ya wengine. Kauli kama “Wewe ni mwanaume,” “Usilie,” au “Vumilia tu” zimekuwa sehemu ya malezi ya wavulana na wanaume.
Lakini nyuma ya maneno hayo kuna swali ambalo mara nyingi halizungumzwi: Mwanaume anapokuwa na maumivu, msongo au matatizo, anamweleza nani?
Matarajio hayo yanaweza kumfanya mwanaume aamini kuwa kuomba msaada ni ishara ya udhaifu, hivyo kuchagua kubeba matatizo yake kimyakimya.
Hali hiyo imeendelea kuibua mjadala kuhusu namna jamii inavyomfundisha mwanaume maana ya kuwa “mwanaume halisi” na madhara yanayoweza kujitokeza pale hisia zinapofichwa kwa muda mrefu.
Utafiti uliofanyika Tanzania kuhusu afya ya akili ya akina baba mjini Mwanza umebaini kuwa takribani akina baba wote waliohusishwa katika utafiti huo walieleza kuwa jukumu lao kuu ni kuwa watoa mahitaji ya familia. Hata hivyo, ukosefu wa ajira na kipato kidogo ulihusishwa na msongo wa kiuchumi, huku baadhi ya wanaume wakihusisha uwezo wa kuitunza familia na uthibitisho wa uanaume wao.

MWANAUME ANAPOFUNDISHWA KUTOKUONESHA HISIA
Michael Baruti, mwandishi wa habari wa Tanzania ambaye ameendesha mazungumzo kuhusu afya ya akili ya wanaume kupitia vipindi vyake mtandaoni, amesema jamii imekuwa ikiwafundisha wanaume kwamba hawapaswi kulia wala kuonyesha hisia.
“Jamii yetu inatuambia kwamba wanaume hawapaswi kulia. Hawapaswi kufunguka na kuwa na hisia,” alisema Baruti.
Baruti alisema changamoto hiyo ilimfanya aanzishe mazungumzo kuhusu afya ya akili ya wanaume baada ya kupitia mwenyewe kipindi kigumu kilichoathiri kazi, familia na mahusiano yake.
Baada ya kupata msaada wa kitaalamu, anasema alianza kuwaeleza marafiki zake kuhusu kile alichokuwa akipitia na kugundua kuwa wanaume wengi walikuwa wakikabili changamoto kama hizo, lakini walikuwa wamezoea kuzichukulia kama sehemu ya maisha kwa sababu tu ni wanaume.
Anasema baadhi ya wanaume wamefundishwa tangu utotoni kwamba wanapaswa kukabiliana na matatizo yao wenyewe na kwamba kushindwa ni jambo lisilokubalika kwa mwanaume. Hata hivyo, anasema mtazamo huo unaweza kuwa sahihi au usiwe sahihi, kutegemea aina na muktadha wa changamoto anayokabiliana nayo mtu.

MTAALAMU: HISIA SI ZA WANAWAKE PEKEE
Nadia Ahmed, mshauri na mwanasaikolojia anayeshiriki katika mijadala kuhusu afya ya akili ya wanaume, amesema hakuna sababu ya kuwazuia wanaume kuonyesha hisia zao kwa sababu hisia ni sehemu ya asili ya binadamu.
“Kibaiolojia, wanaume na wanawake wana mabadiliko ya kikemikali yanayofanana. Wanaume wanaweza kuhisi hisia zote sawa na wanawake, na hilo linadhihirisha kuwa si suala la jinsia, bali ni hisia za kawaida ambazo zinapaswa kushughulikiwa kwa njia yenye afya,” anasema Ahmed.
Ahmed anashauri watu kukubali hisia za huzuni badala ya kuzikataa, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaweza kumsaidia mtu kujenga njia bora za kukabiliana na changamoto.
Mtazamo huo unatoa picha tofauti na dhana kwamba mwanaume anapaswa kuwa mtu asiyeathirika na matatizo. Mwanaume anaweza kuwa mwenye nguvu, mwenye wajibu wa familia na bado akawa na huzuni, hofu au msongo unaohitaji kuzungumziwa.
MAJUKUMU YA KUWA MTOAJI WA FAMILIA
Kwa wanaume wengi, jukumu la kuwa mtoaji wa mahitaji ya familia limekuwa sehemu kubwa ya utambulisho wao. Chakula, kodi, ada za watoto, matibabu na mahitaji mengine yanaweza kuonekana kuwa wajibu ambao mwanaume anapaswa kuhakikisha unapatikana bila kujali hali yake.
Utafiti wa akina baba mjini Mwanza umeonesha kuwa matarajio hayo yanaweza kuhusishwa na msongo wa kiuchumi, hasa pale ambapo mwanaume hana ajira au kipato cha kutosha.
Watafiti walibaini pia kuwa baadhi ya akina baba walihusisha uwezo wa kuwa mtoaji wa familia na maana ya kuwa mwanaume.
Hii ina maana kwamba mwanaume anayeshindwa kutimiza mahitaji yote ya familia anaweza asiwe anakabiliana na tatizo la fedha pekee, bali pia hisia za kushindwa kutimiza kile ambacho jamii imemfundisha kuwa ni wajibu wake.
Changamoto hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi wakati mwanaume hana mtu wa kuzungumza naye kwa sababu anaogopa kuonekana dhaifu au kushindwa.
UKIMYA UNAPOBADILIKA KUWA NJIA YA KUKABILIANA NA MATATIZO
Baruti anasema baadhi ya wanaume wanapokabiliwa na matatizo huamua kuyaficha badala ya kuzungumza, hali ambayo wakati mwingine inaweza kuwafanya kujiingiza katika matumizi ya pombe au dawa za kulevya na tabia nyingine hatarishi zisizosaidia kutatua tatizo lililopo.
Utafiti wa mwaka 2026 uliofanywa na watafiti wanaohusishwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Oslo, pamoja na taasisi nyingine, uliangalia msongo wa akili miongoni mwa wanaume nchini Tanzania.
Utafiti huo ulibaini uhusiano kati ya changamoto za kijamii, unyanyapaa, ukosefu wa msaada wa kijamii na afya ya akili.
Tafiti kama hizi zinaonesha umuhimu wa kulitazama suala la afya ya akili kwa wanaume kwa upana zaidi, badala ya kusubiri tatizo liwe kubwa ndipo msaada utafutwe.
UANAUME SI LAZIMA UJENGWE JUU YA UKIMYA
Ongezeko la mijadala kuhusu afya ya akili ya wanaume linaonyesha kuwa kuna haja ya kuangalia upya baadhi ya mitazamo iliyorithishwa kutoka vizazi vilivyopita.
Mwanaume anaweza kuwa jasiri bila kuficha hisia zake. Anaweza kuwa baba anayewajibika na bado akahitaji msaada. Anaweza kuwa mume anayelinda familia yake na bado akahitaji mtu wa kumsikiliza.
Baruti anasema ni muhimu kuanza mabadiliko hayo tangu utotoni kwa kuacha kuwafundisha wavulana kwamba kulia ni ishara ya kutokuwa mwanaume.
Amesema wazazi wanapaswa kuwauliza watoto wao wanavyojisikia na kuwapa nafasi ya kueleza hisia zao badala ya kuwafundisha kuzificha.
Hili linaweka familia katika nafasi muhimu ya kusaidia kubadilisha mtazamo kuhusu uanaume. Mwanaume anayejua kuwa anaweza kuzungumza na mke wake, mzazi, rafiki au mtaalamu bila kuhukumiwa anaweza kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kukabiliana na changamoto.
MSAADA HAUMFANYI MWANAUME KUWA DHAIFU
Mjadala huu hauhusu kuondoa wajibu wa mwanaume katika familia wala kumfanya asiwe mwajibikaji. Badala yake, unahusu kutambua kwamba wajibu huo unaweza kuwa rahisi zaidi kutekelezwa pale anapokuwa na afya njema ya mwili na akili, akiwa pia na watu anaoweza kuwategemea.
Mwanaume anayesema “Siko sawa” anapokuwa katika hali ngumu si lazima awe ameshindwa. Anaweza kuwa ametambua tatizo mapema na kuchukua hatua ya kutafuta suluhisho.
Kwa mujibu wa Nadia Ahmed, hisia zinapaswa kushughulikiwa kwa njia yenye afya, jambo linalomaanisha kuwa kuzificha si lazima kuwe ishara ya nguvu.
MWISHO WA UKIMYA
Mwanaume si mashine inayotakiwa kufanya kazi bila kuchoka, kulipa gharama bila kulalamika na kukabiliana na kila tatizo bila kuhitaji msaada.
Nyuma ya mwanaume anayeonekana imara kuna mtu mwenye hisia, hofu, matumaini, kushindwa na mafanikio. Kumruhusu mwanaume kuzungumza kuhusu anachopitia hakumvui uanaume; kunampa nafasi ya kuwa binadamu.
Kwa hiyo, huenda wakati umefika wa kuacha kumuuliza mwanaume, “Kwa nini unalia?” na kuanza kumuuliza, “Nini kinakufanya uumie?”
Kwa sababu wakati mwingine, kumsaidia mwanaume hakuanzi kwa kumpa suluhisho. Kunaweza kuanza kwa kumpa nafasi ya kusema ukweli kwamba hayuko sawa.
Leave a comment